TANZANIA YAIMARISHA USHIRIKIANO WA KIBIASHARA NA KENYA, AFRIKA KUSINI
24 Agosti, 2026
Dar es Salaam
Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Kapinga (Mb.), amekutana na kufanya mazungumzo kwa nyakati tofauti na Mabalozi wa Kenya na Afrika Kusini nchini Tanzania, katika Ofisi Ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam, ikiwa ni sehemu ya jitihada za Serikali za kuimarisha mahusiano ya kiuchumi, kibiashara na uwekezaji na nchi hizo.
Katika mazungumzo yake na Balozi wa Kenya nchini Tanzania, Mhe. Catherine Wahome, Waziri Kapinga amejadili namna ya kuendelea kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Kenya, hususan katika sekta za biashara na viwanda. Pande hizo zimebainisha umuhimu wa kuendelea kuweka mazingira wezeshi ya biashara yatakayochochea ukuaji wa biashara baina ya nchi hizo na kuchangia maendeleo ya uchumi.
Aidha, Waziri Kapinga amekutana na Balozi wa Afrika Kusini nchini Tanzania, Mhe. Noluthando Mayende-Malepe, ambapo mazungumzo yao yamejikita katika kuimarisha zaidi ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara kati ya Tanzania na Afrika Kusini, pamoja na kuboresha mazingira yatakayowezesha wafanyabiashara na wawekezaji kutoka pande zote mbili kunufaika na fursa zilizopo.
Mazungumzo hayo yanaendelea kuimarisha nafasi ya Tanzania katika kujenga na kupanua mahusiano ya kibiashara katika masoko ya kikanda na kimataifa.
Akizungumzia umuhimu wa ushirikiano huo, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade), Bw. Ephraim Balozi Mafuru, amebainisha kuwa TanTrade itaendelea kutumia fursa zinazotokana na mahusiano hayo kuwaunganisha wafanyabiashara wa Tanzania na masoko ya Kenya na Afrika Kusini, kuwezesha mikutano ya kibiashara (B2B), pamoja na kutafuta na kupanua masoko ya bidhaa na huduma za Tanzania, hususan bidhaa za Made in Tanzania.