BELARUS YAMWAGA FURSA ZA BIASHARA KWA WATANZANIA KUPITIA TANTRADE
BELARUS YAMWAGA FURSA ZA BIASHARA KWA WATANZANIA KUPITIA TANTRADE
28 Aprili 2026, Dar es Salaam
___________________________________
Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) imeendelea kuimarisha jitihada za kukuza biashara za kimataifa kwa kupokea ugeni kutoka Belarus, hatua inayolenga kuimarisha ushirikiano wa kibiashara na uwekezaji kati ya Tanzania na Belarus.
Katika mazungumzo yaliyofanyika Makao Makuu ya TanTrade jijini Dar es Salaam, pande zote mbili zilijadili kwa kina namna ya kutumia rasilimali na teknolojia zilizopo ili kuendeleza sekta mbalimbali.
Akizungumza kuhusu fursa zilizopo nchini Tanzania, Mkurugenzi Mkuu wa TanTrade, Dkt. Latifa M. Khamis, alisisitiza kuwa Tanzania imebarikiwa na fursa nyingi za biashara katika sekta za madini, kilimo, afya, usafirishaji na burudani. Aliongeza kuwa ushirikiano na Belarus utasaidia kuongeza thamani ya bidhaa za Tanzania na kuimarisha ushindani wake katika masoko ya kimataifa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa National Export Promotion Centre ya Belarus, Mheshimiwa Mikalai Barysevich, alieleza kuwa Belarus imewekeza kwa kiwango kikubwa katika teknolojia za viwandani, hususan mashine za kilimo, vifaa vya afya, na teknolojia za usafirishaji. Alisisitiza kuwa Tanzania inaweza kunufaika kupitia uhamishaji wa teknolojia na utaalamu wa Belarus, jambo litakalosaidia kuongeza uzalishaji na ubora wa bidhaa za ndani.
Mazungumzo haya pia yalihusisha wadau wa sekta binafsi na za umma, ambapo pande zote mbili zilionesha nia ya dhati ya kuanzisha miradi ya pamoja, kubadilishana uzoefu, na kuimarisha mtandao wa biashara kati ya nchi hizi mbili.
Kadhalika, TanTrade ilitumia fursa hiyo kumkaribisha Mhe. Mikalai Barysevich pamoja na wadau wa biashara kutoka Belarus kushiriki katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba 2026) yatakayofanyika kuanzia Juni 28, 2026. Tukio hili kubwa la kitaifa linatarajiwa kuvutia washiriki kutoka zaidi ya nchi 30, na litakuwa jukwaa muhimu la kuonesha bidhaa, huduma na teknolojia mbalimbali.
Ushiriki wa Belarus katika Sabasaba 2026 unatarajiwa kuwa chachu ya kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi, kuongeza uwekezaji wa moja kwa moja, na kuendeleza teknolojia na ubunifu katika sekta mbalimbali za uzalishaji. TanTrade inawahimiza wadau wa ndani kutumia nafasi hii kujipenyeza zaidi katika soko la Ulaya Mashariki na kuimarisha nafasi ya Tanzania katika ramani ya biashara ya kimataifa.