Matembezo ya Kabla ya Maonesho
- June 27, 2026
Dar es Salaam; 27 Juni 2027
Maonesho ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba) yameingia katika historia kwa kuadhimisha miaka 50 tangu kuanzishwa kwake. Sherehe za Jubilei ya Dhahabu zilianza kwa matembezi ya hisani (Walkathon) Juni 27, 2026, yakihusisha mamia ya wananchi, viongozi wa Serikali na wadau wa sekta binafsi. Tukio hili limekuwa ishara ya mshikamano wa kitaifa na uzalendo, sambamba na kuhamasisha matumizi ya bidhaa za ndani na kuimarisha afya ya jamii.
Spika wa Bunge la Tanzania, Mhe. Mussa Azzan Zungu, ndiye aliyekuwa mgeni rasmi na kiongozi wa matembezi hayo. Akihitimisha Walkathon katika Viwanja vya Sabasaba, alisisitiza kuwa maadhimisho haya ni jukwaa muhimu la kuimarisha uzalendo na kuunga mkono bidhaa za Made in Tanzania. Aliongeza kuwa Sabasaba imeendelea kuwa nguzo ya biashara, uwekezaji na ukuaji wa uchumi wa Taifa kwa nusu karne, na kwamba maonesho haya yanapaswa kuendelea kuwa daraja la kuunganisha Watanzania na dunia ya kimataifa.
Mkurugenzi Mkuu wa TanTrade, Dkt. Latifa Khamis Hassan, alishiriki kikamilifu katika matembezi hayo na baadaye kutoa taarifa kuhusu maandalizi ya maonesho ya mwaka huu. Alieleza kuwa TanTrade imejipanga kuhakikisha maonesho ya Jubilei ya Dhahabu yanakuwa ya kipekee, yakionyesha ubunifu, teknolojia na ukuaji wa sekta ya biashara nchini. Aidha, alibainisha kuwa maonesho ya mwaka huu yatakuwa na nafasi kubwa ya kuonyesha bidhaa na huduma za ndani, sambamba na kuimarisha uwekezaji wa kimataifa.
Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Danis Londo, alihudhuria pia katika tukio hilo na kusisitiza dhamira ya Serikali ya kuendeleza sekta ya viwanda kwa kuunga mkono bidhaa za ndani. Alieleza kuwa maonesho ya Sabasaba ni jukwaa muhimu la kuunganisha wazalishaji wa ndani na masoko ya kimataifa, na kwamba Serikali itaendelea kuweka mazingira rafiki ya uwekezaji na biashara. Mhe. Londo alisisitiza kuwa ushiriki wa wananchi na wadau ni msingi wa mafanikio ya sera za viwanda na biashara.
Mwenyekiti wa Bodi ya TanTrade, Prof. Mbamba, alishiriki katika hafla hiyo na kusisitiza umuhimu wa maonesho ya Sabasaba kama chombo cha kukuza biashara na uwekezaji. Alieleza kuwa Bodi ya TanTrade itaendelea kusimamia kwa karibu utekelezaji wa mikakati ya kukuza bidhaa za ndani na kuhakikisha Tanzania inapata nafasi kubwa zaidi katika masoko ya kimataifa. Prof. Mbamba aliongeza kuwa maonesho ya Jubilei ya Dhahabu ni fursa ya kuonyesha safari ya nusu karne ya mafanikio ya sekta ya biashara nchini.
Katika hotuba yake, Dkt. Latifa alimshukuru Spika Zungu, Naibu Waziri Londo na Mwenyekiti wa Bodi Prof. Mbamba kwa kujumuika na wananchi katika tukio hilo. Alisisitiza kuwa ushiriki wa viongozi wa kitaifa ni chachu ya kuhamasisha wadau na wananchi kushiriki kikamilifu. Pia alieleza kuwa maonesho ya mwaka huu yameandaliwa kwa kiwango cha juu, yakilenga kuonyesha mafanikio ya Tanzania katika sekta ya biashara na uwekezaji kwa kipindi cha miaka 50.