Dar es Salaam, 29 Juni 2026
Balozi wa Vietnam nchini Tanzania, Mheshimiwa Vũ Thanh Huyền, leo ametembelea Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (DITF – Sabasaba), akisisitiza nafasi ya maonesho haya kama daraja muhimu la kuunganisha Tanzania katika nyanja za uchumi na diplomasia. Ziara yake imeonesha dhamira ya Vietnam kuongeza ushirikiano na Tanzania katika sekta mbalimbali za kiuchumi, ikiwemo viwanda, biashara na uwekezaji.
Katika mazungumzo yake na Mkurugenzi Mkuu wa TanTrade, Dkt. Latifa Khamis, Balozi Huyền alielezwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amefungua milango ya ushirikiano wa kibiashara kwa misingi ya manufaa kwa pande zote . Hali hii inatoa fursa kwa wananchi kuchangamkia uwezekano wa biashara na uwekezaji, na kuimarisha nafasi ya Tanzania katika uchumi wa kikanda na kimataifa.
Aidha, Balozi alitembelea mabanda mbalimbali ya waoneshaji, akijionea bidhaa, huduma na ubunifu unaoonesha uwezo wa Tanzania katika kukuza uchumi wa ndani na kushirikiana na mataifa rafiki. Ziara yake imethibitisha kuwa DITF 50 si tu maonesho ya biashara, bali ni jukwaa la diplomasia ya kiuchumi linaloimarisha mshikamano wa kimataifa na kuendeleza maendeleo ya viwanda na biashara.
Kwa ujumla, ziara ya Balozi wa Vietnam imetoa taswira ya wazi kuwa DITF 50 ni alama ya ushirikiano wa kikanda na kimataifa, na ni fursa ya kipekee kwa Tanzania kuimarisha nafasi yake katika uchumi wa dunia.