Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania

TanTrade Fostering Business

MAKAMU WA RAIS AHIMIZA TAASISI ZA MUUNGANO KUFANYA KAZI KWA PAMOJA KUWAHUDUMIA WANANCHI

  • September 20, 2026


19 Septemba, 2026, Zanzibar

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius John Ndejembi, amefungua kikao cha Wakuu wa Taasisi za Muungano kilichofanyika katika Ukumbi wa Golden Tulip, Zanzibar, na kuhudhuriwa na viongozi wa taasisi 39.

Mhe. Ndejembi amezitaka taasisi hizo kuimarisha ushirikiano, kubaini na kutumia fursa zilizopo katika pande zote mbili za Muungano, pamoja na kushiriki kwa pamoja katika shughuli mbalimbali ndani na nje ya nchi ili kuongeza tija na manufaa kwa Watanzania.

Amesisitiza umuhimu wa viongozi kuelewa wajibu wao wa kuwahudumia wananchi na kufanya kazi kwa mtazamo wa kujenga “nyumba moja,” huku wakiondoa vikwazo vinavyoweza kudhoofisha ushirikiano na kuhakikisha huduma zinazotolewa zinagusa maisha ya wananchi moja kwa moja.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni, amesema kikao hicho kinalenga kuimarisha ushirikiano kati ya Ofisi ya Makamu wa Rais na Taasisi za Muungano, kuongeza uelewa wa pamoja kuhusu masuala ya Muungano na kuweka mwelekeo wa kuboresha utendaji na ufanisi.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade), Ephraim Balozi Mafuru, ni miongoni mwa viongozi walioshiriki kikao hicho. Kama taasisi ya Muungano, TanTrade ina jukumu la kukuza na kuendeleza biashara Tanzania Bara na Zanzibar kwa kuwaunganisha wafanyabiashara na fursa za masoko, kutoa taarifa za biashara na kutangaza bidhaa za Tanzania ndani na nje ya nchi.

Ushiriki wa TanTrade katika kikao hicho unaimarisha utekelezaji wa majukumu yake katika pande zote mbili za Muungano na kuchochea ushirikiano utakaowawezesha wazalishaji, wafanyabiashara na wajasiriamali kunufaika na fursa za biashara na masoko.