TANZANIA YASHIRIKI MKUTANO MKUU WA 179 WA BIE NCHINI UFARANSA
- November 17, 2026
17 Novemba 2026
Paris, Ufaransa
Tanzania imeshiriki Mkutano Mkuu wa 179 wa Shirika la Kimataifa la Maonesho (Bureau International des Expositions – BIE), uliofanyika tarehe 17 Novemba 2026 jijini Paris, Ufaransa. Ujumbe wa Tanzania umeongozwa na Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Ufaransa, Mhe. Saidi Othman Yakubu, akifuatana na Mkurugenzi wa Ukuzaji Biashara wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade), Bw. Jonathan Nkwabi.
Mkutano huo umewakutanisha wawakilishi wa nchi wanachama kujadili maendeleo ya maandalizi ya maonesho ya kimataifa, ushiriki wa nchi wanachama, pamoja na masuala ya bajeti na utawala wa BIE kwa mwaka 2027. Maonesho yaliyojadiliwa ni Expo 2027 Belgrade nchini Serbia, Expo 2027 Yokohama nchini Japan, Expo 2029 Korat nchini Thailand na Expo 2030 Riyadh nchini Saudi Arabia.
Ushiriki wa Tanzania katika mkutano huo unalenga kuimarisha nafasi ya nchi katika majukwaa ya kimataifa na ushirikiano na nchi wanachama wa BIE. Majukwaa hayo yanatoa fursa za kutangaza bidhaa za Tanzania, kutafuta masoko mapya, kuvutia uwekezaji na kujenga mahusiano ya kibiashara.
Kupitia TanTrade, Serikali inaendelea kuimarisha mikakati ya kutumia maonesho ya kimataifa kuwaunganisha wazalishaji na wafanyabiashara wa Tanzania na wanunuzi kutoka masoko mbalimbali duniani. Juhudi hizo zinalenga kupanua wigo wa masoko ya bidhaa za Tanzania na kutangaza fursa za biashara na uwekezaji zilizopo nchini.