Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania

TanTrade Fostering Business

TANZANIA YAENDELEZA USHIRIKIANO WA KIBIASHARA NA CHINA KUPITIA SERA YA BIASHARA BILA USHURU

  • May 12, 2026


Dar es Salaam, 11 Mei 2026
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade), Dkt. Latifa M. Khamis, amefanya kikao kazi na Wafanyabiashara kutoka kampuni ya Fashion Tourism Investment ya mji wa Yiyan, Hunan nchini China, kwa lengo la kujadili namna ya kuimarisha na kukuza fursa za biashara kati ya Tanzania na China,

Katika kikao hicho kilichofanyika Makao Makuu ya TanTrade jijini Dar es Salaam, TanTrade iliwasilisha kwa kina fursa mbalimbali za kibiashara zinazopatikana nchini Tanzania, ikibainisha maeneo muhimu yenye mvuto wa uwekezaji na biashara, hususan katika sekta za viwanda, kilimo, utalii na huduma. Hatua hii imekusudia kutoa mwongozo wa kitaalamu kwa wadau wa biashara wa China ili kurahisisha maamuzi ya uwekezaji na kuongeza ushirikiano wa kibiashara.

Wafanyabiashara hao walipongeza juhudi za TanTrade chini ya uongozi wa Dkt. Latifa M. Khamis kwa kuwapatia taarifa sahihi na za kina kuhusu mazingira ya biashara nchini Tanzania. Walieleza kuwa hatua hiyo ni chachu ya kuimarisha uhusiano wa kibiashara baina ya pande hizo mbili, na kwamba itarahisisha upatikanaji wa taarifa muhimu kwa wawekezaji wa China wanaotaka kuingia katika soko la Tanzania.

Mazungumzo haya yameelezwa kuwa sehemu ya jitihada za Serikali kupitia TanTrade katika kuimarisha diplomasia ya uchumi na biashara, kwa kutumia fursa ya sera ya Zero Tariff inayotolewa na China kwa bidhaa za Tanzania. Kupitia sera hii, bidhaa za Tanzania zinapata nafasi ya kuingia katika soko la China bila ushuru, jambo linaloongeza ushindani wa bidhaa za Tanzania na kuimarisha mapato ya taifa.

“Tunatambua umuhimu wa kutumia fursa ya Zero Tariff kwa maslahi ya taifa. Mazungumzo haya ni hatua ya kimkakati inayolenga kuimarisha ushirikiano wa kibiashara na kuongeza kasi ya mauzo ya bidhaa za Tanzania katika soko la China. Tunajenga daraja la biashara ambalo litawanufaisha wafanyabiashara wa pande zote mbili,” alisisitiza Dkt. Latifa M. Khamis.
Kwa ujumla, kikao hiki kimeweka msingi wa ushirikiano endelevu kati ya Tanzania na China, kikilenga kuimarisha biashara ya kimataifa, kukuza uwekezaji na kuendeleza diplomasia ya uchumi kwa manufaa ya taifa na wadau wa sekta binafsi.