Serikali
ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeendelea kuthibitisha dhamira yake ya
kukuza biashara na ushirikiano wa kiuchumi na China kupitia mikutano ya wadau
na majukwaa ya kitaalamu yanayolenga kuongeza mauzo ya bidhaa za Tanzania
katika soko la China bila ushuru.
Akihutubia
mkutano wa wadau uliofanyika leo katika Ukumbi wa Johari Rotana, jijini Dar es
Salaam, Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Kapinga (MB),
alisisitiza umuhimu wa kutumia fursa za ushuru nafuu ili kuongeza ushindani wa
bidhaa za Tanzania katika masoko ya kimataifa. Alieleza kuwa hatua hiyo ni
sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuongeza mauzo ya nje, kukuza ajira, na
kuimarisha mapato ya taifa. Aidha, Tanzania imepanga kuanzisha dawati
maalumu la kusaidia wauzaji nje wanaolenga soko la China, kama sehemu ya
mageuzi mapana ya kusaidia wafanyabiashara wa ndani kunufaika na fursa
zinazopanuka za biashara na China.
Waziri
Kapinga pia aliitaka Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania
(TanTrade) kuendelea kuwaunganisha wafanyabiashara wa Tanzania na wenzao
wa China, sambamba na kuhusisha wataalamu wenye ujuzi wa lugha ya Kichina ili
kurahisisha mawasiliano, kuondoa vikwazo vya lugha, na kufungua zaidi fursa za
biashara kwa sekta binafsi na wadau wa viwanda.
Kwa
upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TanTrade, Dkt. Latifa Khamis, alisisitiza
dhamira ya taasisi hiyo ya kuendelea kuwa daraja la biashara kati ya Tanzania
na masoko ya kimataifa. Alieleza kuwa TanTrade imejipanga kutoa msaada wa
kitaalamu kwa wafanyabiashara wa ndani ili kuhakikisha mawasiliano na majadiliano ya kibiashara yanakuwa
na ufanisi mkubwa. Dkt. Khamis aliongeza kuwa TanTrade itaendeleza majukwaa ya
ushirikiano wa moja kwa moja kati ya wafanyabiashara wa Tanzania na wenzao wa
China, kwa lengo la kuongeza mtiririko wa bidhaa na uwekezaji.
Mkutano
huo ulihudhuriwa na wadau mbalimbali wa sekta ya viwanda na biashara, ambapo
washiriki walipongeza juhudi za Serikali na TanTrade katika kuhakikisha bidhaa
za Tanzania zinapata nafasi kubwa zaidi katika soko la China, kwa manufaa ya
taifa na wananchi wake