TANZANIA NA SWEDEN KUIMARISHA BIASHARA NA UWEKEZAJI KATIKA SEKTA ZA KIMKAKATI
- October 12, 2026
13 Oktoba 2026, Dar es Salaam
Tanzania na Sweden zimeendelea kuimarisha ushirikiano wa kibiashara na uwekezaji katika sekta za kimkakati za maji, nishati na miundombinu, huku wafanyabiashara wa nchi hizo wakihimizwa kuanzisha ubia utakaopanua uzalishaji, masoko na fursa za kiuchumi. Msisitizo huo umetolewa katika semina ya biashara iliyofanyika jijini Dar es Salaam, ikiwakutanisha wawakilishi wa makampuni ya Sweden na wadau mbalimbali wa maendeleo.
Akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Viwanda na Biashara, Mkurugenzi wa Ukuzaji Biashara wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade), Bw. Jonathan Nkwabi, amesema mahusiano mazuri kati ya Tanzania na Sweden ni msingi muhimu wa kupanua biashara na uwekezaji. Amehimiza makampuni ya nchi hizo kuendeleza ushirikiano kwa vitendo kupitia ubia unaotumia teknolojia, utaalamu na rasilimali zilizopo kuongeza uzalishaji na ushindani.
Nkwabi ameeleza kuwa, kupitia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Tanzania inalenga kujenga uchumi wenye thamani ya dola za Marekani trilioni moja na kufikia wastani wa kipato cha dola za Marekani 7,000 kwa mtu. Kufikia malengo hayo kunahitaji uwekezaji unaoleta mageuzi, msingi imara wa viwanda vyenye ushindani na ushiriki mpana wa sekta binafsi. Amesisitiza kuwa nishati ya uhakika na mifumo endelevu ya usimamizi wa maji ni muhimu katika kupanua viwanda, kuimarisha minyororo ya thamani ya mazao ya kilimo na kuongeza ajira.
Kwa upande wake, Balozi wa Tanzania nchini Sweden, Mhe. Swahiba Mndeme, amezihimiza kampuni za Sweden kuchangamkia fursa za uwekezaji nchini, ikiwemo kushiriki misafara ya kibiashara ili kutambua maeneo ya ushirikiano na kukutana na wabia. Aidha, amewahimiza wafanyabiashara wa Tanzania kutumia mahusiano hayo kuanzisha ubia, kujifunza teknolojia mpya na kupanua masoko ya bidhaa na huduma zao.
Takwimu za mwaka 2025 zinaonesha kuwa biashara ya bidhaa kati ya Tanzania na Sweden ilifikia takribani dola za Marekani milioni 68.6, ambapo Tanzania iliuza bidhaa zenye thamani ya dola za Marekani milioni 3.3 na kuagiza bidhaa zenye thamani ya dola za Marekani milioni 65.3 kutoka Sweden. Takwimu hizo zinaonesha nafasi ya kuongeza mauzo ya bidhaa za Tanzania katika soko la Sweden kupitia uwekezaji katika uzalishaji, uongezaji thamani na uunganishaji wa wafanyabiashara na wanunuzi.
Semina hiyo imehudhuriwa na wawakilishi wa makampuni saba ya Sweden yanayojihusisha na sekta za maji, nishati na miundombinu, pamoja na wadau wengine wa maendeleo. Kupitia jukwaa hilo, TanTrade inaendeleza jukumu lake la kuunganisha wafanyabiashara na fursa za masoko na ushirikiano, huku majadiliano yakilenga kutambua maeneo ya uwekezaji yenye manufaa kwa nchi zote mbili, ikiwemo fursa zilizopo Zanzibar na Dodoma.