Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania

TanTrade Fostering Business

TANZANIA NA KENYA ZATIA SAINI MIKATABA NANE, ZAKUBALIANA KUONDOA VIKWAZO VYA BIASHARA

  • May 4, 2026

TANZANIA NA KENYA KUONDOA VIKWAZO VYA BIASHARA NA KUIMARISHA USHIRIKIANO WA KIBIASHARA

Dar es Salaam, 04 Mei 2026

Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) inapongeza hatua kubwa ya kihistoria iliyofikiwa leo Ikulu Dar es Salaam, ambapo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, na Rais wa Jamhuri ya Kenya, Mheshimiwa William Samoei Ruto, wameshuhudia utiaji saini wa mikataba nane ya ushirikiano kati ya nchi hizi mbili.

Makubaliano haya yamejikita katika sekta muhimu za biashara, uwekezaji, nishati, kilimo, miundombinu, utalii, Tehama, ulinzi na usalama, na yanatoa dira mpya ya kuimarisha uhusiano wa kibiashara na kiuchumi kati ya Tanzania na Kenya. TanTrade tunaona hatua hii kama msingi wa kuondoa vikwazo visivyo vya kikodi, kuimarisha Kamati za Pamoja za Biashara, na kujenga mazingira bora ya wafanyabiashara na wawekezaji wa pande zote mbili.

Katika sekta ya nishati na miundombinu, makubaliano haya yamegusia miradi ya kuunganisha mifumo ya umeme, bomba la gesi asilia, reli kupitia Tanga–Moshi–Kilimanjaro–Taveta, pamoja na ukanda wa barabara ya Dar es Salaam–Bagamoyo–Pangani–Tanga–Horohoro hadi Mombasa. Hatua hizi zitafungua fursa mpya za biashara, kuongeza ufanisi wa usafirishaji na kuimarisha ushindani wa kikanda.

Aidha, mikataba iliyosainiwa imejumuisha maeneo ya reli, upembuzi yakinifu wa bomba la gesi asilia kutoka Dar es Salaam hadi Mombasa, usaidizi wa kisheria katika makosa ya jinai, kilimo, utambuzi wa vyeti vya mabaharia, usimamizi wa usafiri wa majini, viwango kati ya Zanzibar na Kenya, pamoja na kujengeana uwezo katika utumishi wa umma.

Katika Kongamano la Biashara na Uwekezaji lililoshirikisha viongozi wa serikali na sekta binafsi, TanTrade tunaunga mkono kikamilifu maazimio ya kuondoa vikwazo vya biashara, kurekebisha sheria na mifumo inayokwamisha uwekezaji, na kujenga miundombinu ya kurahisisha biashara kati ya Tanzania na Kenya.

Mkurugenzi Mkuu wa TanTrade, Dkt. Latifa Mohamed Khamis, ametoa wito kwa Watanzania wote kutumia kikamilifu fursa za biashara na uwekezaji zinazotokana na makubaliano haya, akisisitiza kuwa Tanzania na Kenya ni washirika wa kibiashara wanaohitajiana na kutegemeana, hivyo ni wakati muafaka wa sekta binafsi na wananchi kushiriki kikamilifu katika kukuza uchumi wa kikanda.

TanTrade itaendelea kuwa daraja la biashara kati ya Tanzania, Kenya na Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa ujumla, kuhakikisha makubaliano haya yanatafsiriwa katika manufaa ya moja kwa moja kwa wafanyabiashara na wananchi.