Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania

TanTrade Fostering Business

TANTRADE YAWAHIMIZA WAFANYABIASHARA KUTUMIA MAONESHO YA 27 YA AUTOEXPO AFRICA KUPANUA MASOKO

  • November 18, 2026

18 Novemba 2026
Dar es Salaam

Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) imewahimiza wafanyabiashara kutumia fursa zinazopatikana katika maonesho mbalimbali ili kukuza biashara na kupanua masoko ya bidhaa wanazozalisha.

Kauli hiyo imetolewa leo, 18 Novemba 2026, wakati wa ufunguzi wa Maonesho ya 27 ya AUTOEXPO AFRICA yanayofanyika katika Ukumbi wa Diamond Jubilee, jijini Dar es Salaam, kuanzia 18 hadi 20 Novemba 2026.

Mwakilishi wa TanTrade, Meneja wa Masoko ya Ndani na Nje ya Nchi, Bi. Doroth Urio ameeleza kuwa TanTrade inaendelea kuwa kiungo muhimu kati ya wafanyabiashara na masoko kwa kuwezesha mazingira ya kukutana na wateja, kujenga ushirikiano na kutambua fursa mpya za biashara.

Aidha, ameeleza kuwa maonesho ya AutoExpo Africa ni zaidi ya jukwaa la kuonesha magari, vipuri na vifaa mbalimbali vya magari, kwani yanatoa nafasi kwa wafanyabiashara wa sekta tofauti kukutana, kubadilishana uzoefu na kujifunza mbinu mbalimbali za kuimarisha shughuli zao za kibiashara ikiwemo thamani ya bidhaa na namna bora kuwa na vifungashio bora kwenye bidhaa zinazozalishwa nchini.

TanTrade inaendelea kusisitiza umuhimu wa wafanyabiashara kutumia maonesho ya ndani na kimataifa vyema ili kufikia wateja wapya, kutangaza huduma na bidhaa ili kupanua fursa za uwekezaji na ushirikiano wa kibiashara.