TANTRADE YAUNGA MKONO UWEZESHAJI WANAWAKE KATIKA BIASHARA KUPITIA MALKIA WA NGUVU 2026
- November 14, 2026
14 Novemba 2026
Dar es Salaam
Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) imeshiriki katika hafla ya kilele cha Malkia wa Nguvu 2026, iliyofanyika tarehe 14 Novemba 2026 katika Ukumbi wa Ocean View Arena, Kawe, jijini Dar es Salaam. Ushiriki huo ni sehemu ya juhudi za Mamlaka za kuunga mkono uwezeshaji wa wanawake na kuhamasisha ushiriki wao katika biashara, ujasiriamali na shughuli nyingine za kiuchumi.
Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, ambaye alikuwa mgeni rasmi, ameipongeza Clouds Media Group kwa kuwawezesha wanawake na kusaidia makundi yenye uhitaji kupitia jukwaa la Malkia wa Nguvu. Amesisitiza umuhimu wa kuendeleza juhudi hizo ili kuwafikia wanufaika wengi zaidi.
Aidha, Mhe. Dkt. Nchemba amemtaja Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuwa Malkia wa Nguvu, akirejea juhudi za Serikali katika kuimarisha elimu ya mtoto wa kike, ikiwemo ujenzi wa shule za wasichana katika kila mkoa. Ameeleza kuwa hatua ya kuruhusu wanafunzi waliokatiza masomo kutokana na ujauzito kurejea shuleni imewapa fursa nyingine ya kuendelea na elimu na kutimiza ndoto zao.
Ushiriki wa TanTrade katika jukwaa hilo unaonesha dhamira ya Mamlaka ya kuunga mkono uwezeshaji wa wanawake kiuchumi kupitia biashara na ujasiriamali. Kupitia majukumu yake ya kutoa elimu ya biashara, taarifa za masoko na kuwaunganisha wazalishaji na wanunuzi, TanTrade inaendelea kuhamasisha wanawake kutumia uwezo na ubunifu wao kukuza biashara na kuchangia maendeleo ya Taifa.