TANTRADE WANAWAKE WAJITOLEA KWA WATOTO YATIMA
- March 16, 2026
TANTRADE WANAWAKE WAJITOLEA KWA WATOTO YATIMA
Dar es Salaam, Machi 15, 2026
______________
Wafanyakazi wa kike wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) wameonyesha mshikamano na huruma kwa jamii kwa kuandaa futari ya pamoja na watoto yatima wa kituo cha TCS na Salama Orphance Centre. Sambamba na hilo, wamekabidhi msaada wa vifaa muhimu ikiwemo kompyuta na mashine ya kutolea nakala, vinavyotarajiwa kusaidia shughuli za kituo na kuimarisha elimu ya watoto wanaolelewa hapo.
Aidha, ujumbe wa wawakilishi hao uliambatana na salamu kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa TanTrade, Dkt. Latifa Khamis, ambaye aliahidi kuendeleza mahusiano kati ya Taasisi yake na vituo vya kulelea watoto yatima na kuwahusia kuzingatia malezi bora wanayopewa, elimu, na kumtegemea Mungu ili kufanikisha ndoto zao.
Kwa upande wake, msimamizi wa kituo, Bw. Saidi Kasela, alitoa shukrani za dhati kwa msaada huo, akieleza kuwa utasaidia kutunza kumbukumbu na kuongeza fursa za kujifunza. Aliwaomba wadau wengine kuendelea kushirikiana na kituo, akisisitiza kuwa watoto yatima ni taifa la kesho na wanahitaji msaada na fursa bora ili kufanikisha malengo ya maisha.