TANTRADE YAHIMIZA SEKTA YA MADINI KUKUMBATIA ALAMA YA “MADE IN TANZANIA”
- October 4, 2026
3 Oktoba 2026
Geita
Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) imewahimiza wachimbaji na wafanyabiashara katika mnyororo wa thamani wa madini kutumia alama ya kitaifa ya “Made in Tanzania” ili kuimarisha utambulisho na mwonekano wa bidhaa katika masoko ya ndani na ya kimataifa.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TanTrade, Meneja wa Maendeleo ya Biashara Bw. Deo Shayo ameitaka sekta ya madini kuhakikisha utambulisho wa Tanzania unaonekana katika masoko ya dunia. Amesisitiza kuwa kuunganisha alama ya “Made in Tanzania” na shughuli za kuongeza thamani kutasaidia bidhaa za madini kujitofautisha, kuimarisha utambulisho wa asili yake na kufungua fursa za masoko mapya.
Bw. Shayo alitoa kauli hiyo wakati wa hafla ya kufunga Maonesho ya Tisa ya Teknolojia ya Madini yaliyofanyika katika Viwanja vya Dr. Samia Suluhu Hassan, Geita, na kufungwa rasmi na Waziri Mkuu Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba.