TANTRADE KUFUNGUA MASOKO YA KIMATAIFA KWA HUDUMA ZA TANZANIA
- September 28, 2026
Doha, Qatar, 27 Septemba, 2026
Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) imepewa jukumu la kuimarisha biashara ya huduma katika masoko ya kimataifa kwa kutambua na kukuza fursa zilizopo katika sekta mbalimbali, zikiwemo huduma za kitaalamu na rasilimali watu.
Maelekezo hayo yametolewa na Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Kapinga, wakati wa ziara ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba, katika Kampuni ya Usafirishaji ya MOWASALAT inayomilikiwa na Serikali ya Qatar. Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Kapinga na Mkurugenzi Mkuu wa TanTrade, Bw. Ephraim Balozi Mafuru, ni miongoni mwa viongozi walioshiriki katika ziara hiyo.
Akiongea katika ziara hiyo Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Kapinga amesisitiza kuwa biashara ya kimataifa haipaswi kujikita katika mauzo ya bidhaa pekee, bali inapaswa kujumuisha pia huduma zinazoweza kutolewa na Watanzania katika masoko ya nje. Ametaja ajira za vijana wa Kitanzania kuwa miongoni mwa maeneo yenye fursa kubwa ya kuchangia ukuaji wa biashara ya huduma na uchumi wa Taifa.
Ameipongeza MOWASALAT kwa kutoa ajira kwa vijana 722 wa Kitanzania, hatua inayowawezesha kujipatia kipato, kukuza ujuzi na kupata uzoefu katika soko la ajira la kimataifa.
Katika kutekeleza jukumu hilo, TanTrade itashirikiana na wadau mbalimbali kutambua fursa za huduma katika masoko ya kimataifa, kuwaunganisha watoa huduma wa Tanzania na masoko hayo, pamoja na kuongeza mchango wa sekta ya huduma katika kukuza biashara, ajira na mapato ya Taifa.
Aidha, majadiliano yaliyofanyika yameonesha umuhimu wa kuwakutanisha wafanyabiashara wa Tanzania na Qatar kupitia taasisi zao za uwakilishi, zikiwemo QCCI, TPSF na TNCC, ili kujadili maeneo ya ushirikiano wa kimkakati katika biashara na uwekezaji.
Ushiriki wa TanTrade katika ziara hiyo unaimarisha juhudi za Tanzania za kupanua wigo wa biashara ya bidhaa na huduma katika masoko ya kimataifa, sambamba na kukuza fursa za ajira, uwekezaji na ushirikiano wa kibiashara kati ya Tanzania na Qatar.