TANTRADE KUWAWEZESHA VIJANA KUNUFAIKA NA FURSA ZA BIASHARA KATIKA MAONESHO YA OSBORNS 2026
- October 12, 2026
12 Oktoba, 2026, Dar es Salaam
Mamlaka ya Maendeleo ya biashara Tanzania (TanTrade) imesema itashirikiana na waandaaji wa Maonesho ya Osborns Exhibition 2026 kuwawezeha vijana kwa kuwaunganisha wajasiriamali na wafanyabiashara wadogo na fursa za biashara kupitia huduma ya Kliniki ya biashara, itakayowezesha upatikanaji wa taarifa za masoko, ushauri wa kitaalamu na mbinu za kukuza biashara.
Kauli hiyo imetolewa kufuatia kikao kati ya uongozi wa TanTrade na waandaaji wa maonesho hayo, kilicholenga kuweka mikakati ya pamoja kuelekea maonesho yanayotarajiwa kufanyika kuanzia tarehe 27 hadi 31 Oktoba 2026 katika viwanja vya Kijitonyama Posta, jijini Dar es Salaam. Maonesho hayo yanatarajiwa kuwakutanisha taasisi za serikali, sekta binafsi na wazalishaji wa bidhaa za Kitanzania.
Katika kikao hicho, waandaaji wa maonesho hayo wameiomba TanTrade kushiriki kwa kutoa huduma ya Kliniki ya biashara itakayowasaidia vijana kupata maarifa ya kuanzisha na kuendeleza biashara, kuboresha bidhaa na huduma, kutambua fursa za masoko na kutatua changamoto zinazokwamisha ukuaji wa biashara zao.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa TanTrade, Bi. Lulu Mkudde, amesema ushiriki wa TanTrade katika maonesho hayo ni sehemu ya juhudi za Mamlaka za kukuza biashara za ndani, kuimarisha ushindani wa bidhaa za Kitanzania na kuwaunganisha wazalishaji na masoko.
Ameongeza kuwa Kliniki ya biashara itatoa fursa kwa vijana na wajasiriamali kupata ushauri na taarifa zitakazowawezesha kufanya maamuzi sahihi ya kibiashara, kutumia fursa zilizopo na kukuza biashara zao kwa tija.