TANTRADE YAIMARISHA MAHUSIANO YA BIASHARA NA UWEKEZAJI KATIKA JUKWAA LA EU–TANZANIA NCHINI ITALIA
- October 4, 2026
3 Oktoba 2026, Italia
Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) imeshiriki katika Jukwaa la Uwekezaji na Biashara kati ya Umoja wa Ulaya na Tanzania pamoja na ziara ya kutangaza fursa (EU–Tanzania Investment and Business Forum and Roadshow) nchini Italia, likilenga kuimarisha mahusiano ya biashara, uwekezaji na ushirikiano wa kiuchumi kati ya Tanzania na nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya (EU).
TanTrade imewakilishwa na Mkurugenzi wa Ukuzaji Biashara, Bw. Jonathan M. Nkwabi, aliyeshiriki katika mjadala wa jopo kuhusu kuunganisha wafanyabiashara wa Tanzania na wawekezaji pamoja na wanunuzi wa kimataifa, hususan kutoka masoko ya Umoja wa Ulaya.
Katika mjadala huo, Bw. Nkwabi ameeleza kuwa upanuzi wa masoko, uongezaji thamani, uhamishaji wa teknolojia na ubunifu ni maeneo muhimu ya kukuza biashara na kuvutia uwekezaji nchini. Amesisitiza kuwa mahitaji na viwango vya masoko ya kimataifa yanapaswa kutumiwa kama fursa ya kuimarisha uwezo wa biashara za Tanzania kupitia uwekezaji katika ubora, mifumo ya ufuatiliaji wa bidhaa, teknolojia na uzalishaji endelevu.
Aidha, amebainisha kuwa TanTrade inaunganisha wafanyabiashara wa Tanzania na wanunuzi, wawekezaji, watoa teknolojia na washirika wa kimkakati kupitia mikutano ya biashara baina ya wafanyabiashara (B2B), majukwaa na ziara za biashara pamoja na utoaji wa taarifa za masoko. Hatua hizo zinalenga kujenga mahusiano ya kudumu yanayoweza kuzaa mikataba, ubia, uwekezaji na fursa mpya za biashara.
Bw. Nkwabi pia amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya Serikali, sekta binafsi, taasisi za maendeleo na washirika wa kimataifa katika kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji. Ushirikiano huo ni muhimu katika kuwezesha biashara ndogo na za kati kupata maarifa, mitaji, teknolojia na masoko.
Ushiriki wa TanTrade katika jukwaa hilo unaendeleza juhudi za kufungua masoko na kuimarisha ushirikiano wa wafanyabiashara wa Tanzania na washirika wa Umoja wa Ulaya, huku ukilenga kuongeza ushindani wa bidhaa na huduma za Tanzania katika minyororo ya thamani ya kikanda na kimataifa.