TANTRADE KUIMARISHA BIASHARA ZA KIKANDA KUPITIA BANDARI KAVU YA KWALA
- September 9, 2026
9 SEPTEMBA, 2026; PWANI.
Katika kuimarisha uelewa wa fursa za biashara na uwekezaji, TanTrade imewawezesha washiriki wa Kongamano la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Malawi kutembelea Bandari Kavu ya Kwala, Pwani, kwa ajili ya kujifunza namna miundombinu ya usafirishaji inavyosaidia kurahisisha biashara.
Wakati wa ziara hiyo, washiriki walijifunza kuwa Bandari Kavu ya Kwala hupokea, kuhifadhi na kusafirisha mizigo kwenda maeneo mbalimbali ndani na nje ya Tanzania, ikiwemo DRC Congo, Malawi, Burundi na Zambia. Mizigo inayohudumiwa ni pamoja na magari, vyakula, nafaka na kemikali za kilimo.
Ziara hiyo iliwapa washiriki fursa ya kuona kwa vitendo mchango wa Kwala katika kupunguza foleni za malori jijini Dar es Salaam, kuongeza ufanisi wa usafirishaji na kuiwezesha Serikali kupata mapato kupitia shughuli mbalimbali zinazofanyika bandarini, hatua inayochochea biashara na uwekezaji kati ya Tanzania na nchi jirani.