Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania

TanTrade Fostering Business

WATUMISHI WA TANTRADE WANOLEWA KUHUSU MASUALA YA AFYA ILI KUIMARISHA USTAWI MAHALI PA KAZI

  • May 7, 2026

WATUMISHI WA TANTRADE WANOLEWA KUHUSU MASUALA YA AFYA ILI KUIMARISHA USTAWI MAHALI PA KAZI

Dar es Salaam, 06 Mei 2026

Watumishi wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) wamepatiwa mafunzo kuhusu masuala ya afya kwa lengo la kuimarisha ustawi wao mahali pa kazi na kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya kila siku.
Mafunzo hayo yamegusa mada muhimu ikiwemo mbinu za kujikinga na magonjwa ya kuambukiza kama VVU/UKIMWI na Kifua Kikuu, pamoja na magonjwa yasiyoambukiza. Aidha, watumishi walielimishwa kuhusu umuhimu wa afya ya akili kama sehemu ya ustawi wa jumla wa mfanyakazi.

Katika mafunzo hayo, watumishi walihimizwa kuzingatia upimaji wa afya mara kwa mara, kufuata lishe bora, na kujenga utamaduni wa kufanya mazoezi ya mwili. Pia walihimizwa kutumia kituo cha mazoezi (Gym) kilichopo eneo la kazi ili kuimarisha afya zao.

Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Mkurugenzi Mkuu wa TanTrade, Dkt. Latifa Mohamed Khamis, alisisitiza kuwa uwekezaji katika afya za watumishi ni msingi wa kujenga team bora yenye ufanisi wa kazi na afya imara. Alieleza kuwa taasisi yenye watumishi wenye afya njema huongeza tija, ubunifu na mshikamano, hivyo kuimarisha maendeleo ya TanTrade na taifa kwa ujumla.

Mafunzo yametolewa na wataalam wa afya kutoka Hospitali ya Rufaa ya Halmashauri ya Manispaa ya Temeke, jijini Dar es Salaam, ambao wamesisitiza kuwa uwekezaji katika afya za watumishi ni msingi muhimu wa kuongeza tija na maendeleo ya taasisi.