TANTRADE YAPOKEA UJUMBE WA WAWEKEZAJI KUTOKA CHINA KUTAFUTA FURSA ZA BIASHARA NA VIWANDA
- August 24, 2026
24 Agosti, 2026
Dar es Salaam
Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade), leo Agosti 24, 2026, imepokea ujumbe wa wafanyabiashara na wawekezaji kutoka China-Africa Industrial Forum (CAIF) katika Makao Makuu ya TanTrade jijini Dar es Salaam, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kutafuta na kuendeleza fursa za biashara, uwekezaji na ushirikiano wa viwanda kati ya Tanzania na China.
Ujumbe huo umeongozwa na Bw. Cheng Zhigang, Katibu Mkuu wa China-Africa Industrial Forum, na unajumuisha wawakilishi wa makampuni yanayojihusisha na sekta mbalimbali ikiwemo teknolojia, kilimo, viwanda, biashara na uwekezaji. Ziara hiyo imelenga kujifunza zaidi kuhusu mazingira ya biashara na uwekezaji nchini Tanzania, pamoja na kubaini maeneo ya ushirikiano yanayoweza kuunganisha makampuni ya China na wafanyabiashara na wazalishaji wa Tanzania.
Miongoni mwa maeneo yaliyojadiliwa ni fursa katika sekta ya usafirishaji na ugavi (logistics), uendelezaji wa maeneo ya viwanda (industrial parks), kilimo na uchakataji wa mazao, teknolojia pamoja na uwekezaji katika viwanda. Maeneo hayo yanatoa fursa ya kujenga ushirikiano utakaosaidia kuongeza thamani ya bidhaa zinazozalishwa nchini, kuimarisha minyororo ya thamani na kufungua fursa zaidi za biashara na uwekezaji.
Ziara hiyo inakuja wakati ushirikiano wa kibiashara kati ya Tanzania na China ukiendelea kukua. Mwaka 2025, thamani ya biashara baina ya nchi hizo mbili ilifikia takribani Dola za Marekani bilioni 11.28, ikiwa ni ongezeko la asilimia 27 ikilinganishwa na mwaka uliotangulia. China pia imeendelea kuwa miongoni mwa washirika wakubwa wa Tanzania katika biashara na uwekezaji.
Kupitia ziara hiyo, TanTrade inaendelea kutekeleza jukumu lake la kukuza na kuwezesha biashara kwa kuwaunganisha wafanyabiashara na wazalishaji wa Tanzania na washirika wa kimataifa, kutafuta masoko mapya, kuwezesha mahusiano ya kibiashara (B2B) na kuvutia ushirikiano wenye tija katika sekta za uzalishaji na viwanda. Ushirikiano na ujumbe huo unatarajiwa kufungua milango zaidi kwa bidhaa na huduma za Tanzania, ikiwemo Made in Tanzania, kuingia katika masoko ya China na kuimarisha biashara baina ya nchi hizo mbili.