TANTRADE YATOA HUDUMA ZA KUKUZA NA KUENDELEZA BIASHARA KWA WANANCHI WA ARUSHA
- September 19, 2026
18 Septemba, 2026
Arusha
Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) inaendelea kutoa huduma mbalimbali kwa wananchi kupitia Kliniki ya Viwanda na Biashara inayofanyika katika Viwanja vya Ngarenaro, jijini Arusha, kuanzia tarehe 14 hadi 19 Septemba, 2026. Kliniki hiyo imeandaliwa na Wizara ya Viwanda na Biashara kwa kushirikiana na taasisi zilizo chini yake.
Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Mhe. Modest Mkude, leo ametembelea banda la TanTrade na kujionea huduma zinazotolewa kwa wazalishaji, wafanyabiashara na wajasiriamali wa Mkoa wa Arusha.
Maafisa wa TanTrade wamemueleza Mkuu wa Wilaya kuwa, kupitia Kliniki hiyo, TanTrade inatoa huduma za utafutaji na ukuzaji wa masoko, utangazaji wa bidhaa zenye nembo ya “Made in Tanzania," kuwaunganisha wazalishaji na wanunuzi wa ndani na nje ya nchi, kutoa taarifa kuhusu biashara na masoko, pamoja na kuwawezesha wafanyabiashara kushiriki katika maonesho ya biashara ya ndani na kimataifa.
Ushiriki wa TanTrade unalenga kuwasaidia wananchi kupata masoko ya uhakika, kuongeza thamani na ubora wa bidhaa zao na kuimarisha ushindani katika masoko ya ndani, kikanda na kimataifa.
Wananchi, wazalishaji, wafanyabiashara na wajasiriamali mnakaribishwa kutembelea banda la TanTrade katika Viwanja vya Ngarenaro, Arusha, ili kupata huduma, elimu na taarifa kuhusu fursa mbalimbali za biashara na masoko.