Dar es Salaam, 4 Agosti 2026
Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) imeungana na wadau wa mazingira na plastiki katika kikao kilichofanyika jijini Dar es Salaam, kikihusisha wawakilishi wa sekta ya umma, sekta binafsi, wazalishaji na wadau wa mazingira. Kikao hicho kililenga kujadili namna ya kukuza biashara ya plastiki na vifungashio kwa njia endelevu bila kuathiri mazingira, na kilifanyika katika Ukumbi wa Ubungo Plaza.
Mkutano huo uliandaliwa na Ofisi ya Makamu wa Rais – Mazingira, ukiongozwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Mheshimiwa Mhandisi Hamad Yussuf Masauni (MB), pamoja na Waziri wa Viwanda na Biashara, Mheshimiwa Judith Kapinga (MB).
Katika hotuba yake, Waziri Kapinga alisisitiza kuwa viwanda vinavyozalisha bidhaa za plastiki vinapaswa kuwa na mikakati thabiti ya kutunza mazingira kabla ya kuanza miradi ya uzalishaji. Aliongeza kuwa sekta binafsi inapaswa kuwa kinara katika kutatua changamoto za mazingira kwa kutumia teknolojia na ubunifu wa kisasa, kwakuwa teknolojia inaletwa na sekta binafsi, na kuweka bayana kuwa ushirikiano wa karibu kati ya serikali na sekta binafsi ni muhimu ili kulinda mazingira kwa manufaa ya vizazi vijavyo.
Kwa upande wake, Bw. Ephraim Mafuru, Mkurugenzi Mkuu wa TanTrade, alieleza kuwa TanTrade kama mamlaka inayosimamia mustakabali wa biashara nchini, imejikita kuhakikisha sekta ya biashara inapata uelewa wa utunzaji mazingira. Alifafanua kuwa masoko ya kimataifa yanahitaji mpango kazi wa mazingira, na bila kuzingatia hilo wafanyabiashara wa Tanzania hawawezi kunufaika kikamilifu na fursa za kimataifa.
Aidha, wazalishaji wa Kitanzania wamekumbushwa kusajili bidhaa zao na kutumia Nembo ya Taifa ya “Made in Tanzania” inayotolewa na TanTrade, ili kurahisisha upatikanaji wa masoko ya kimataifa na kuongeza ushindani wa bidhaa za ndani.
Kikao hiki kimekuwa jukwaa muhimu la kuunganisha wadau wa sekta binafsi na serikali katika kujadili sera, mikakati na teknolojia mbadala za vifungashio rafiki kwa mazingira. Hatua hii inatarajiwa kuimarisha taswira ya Tanzania kimataifa, kukuza biashara endelevu na kulinda mazingira kwa manufaa ya taifa na dunia kwa ujumla.