Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania

TanTrade Fostering Business

TANTRADE YASHIRIKI KONGAMANO LA KUWEZESHA WANAWAKE

  • April 13, 2026

TANTRADE YASHIRIKI KONGAMANO LA KITCHEN PARTY GALA

Dar es Salaam, 12 Aprili 2026
___________________________________________________________
Watumishi wanawake wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) wameshiriki katika Kongamano la Kitchen Party Gala lililofanyika katika ukumbi wa Mlimani City, jijini Dar es Salaam. Kongamano hili, pamoja na mambo mengine, lina lengo la kumjengea mwanamke ujasiri katika biashara na masuala ya kiuchumi, huku likitoa fursa ya kujifunza, kubadilishana uzoefu na kupata maarifa yatakayomwezesha kukuza shughuli zake za kiuchumi.

Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Kapinga, kama mlezi wa biashara nchini Tanzania, amepongeza kufanyika kwa kongamano hilo na kusisitiza umuhimu wa wanawake kulitumia kama jukwaa la kukuza na kupanua biashara zao. Amesema majukwaa kama haya ni nyenzo muhimu katika kuongeza ushiriki wa wanawake katika uchumi na kuimarisha sekta ya biashara nchini. Aidha, amezipongeza taasisi mbalimbali zilizoshiriki, ikiwemo TanTrade, kwa mchango wao katika maendeleo ya sekta hiyo.

Kwa upande wake, msimamizi wa kongamano hilo na kiongozi wa jukwaa, Dina Marios, ameipongeza TanTrade kwa mchango wake katika kufanikisha tukio hilo. Aidha, aliwakumbusha wanawake kushiriki kikamilifu katika Maonesho ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), ambayo mwaka huu yanatimiza miaka 50 tangu kuanzishwa kwake.

Aidha, uongozi wa TanTrade umetoa shukrani kwa waandaaji wa kongamano hilo kwa kutambua mchango wa taasisi hiyo. Kupitia jukwaa hilo, TanTrade pia ilitoa elimu kuhusu Maonesho ya Sabasaba na kueleza namna wanawake wanavyoweza kunufaika na fursa mbalimbali zinazotolewa, ikiwemo kupanua masoko na kukuza biashara zao. Sambamba na hilo, wanawake walielimishwa kuhusu rajam ya taifa ya “Made in Tanzania”, inayolenga kutambulisha bidhaa za Tanzania na kuziongezea fursa za masoko ya kimataifa, hivyo kuwataka kuitumia vyema katika kupanua masoko ya biashara zao. Hatua hizi zinaendana na dira ya taifa ya kujenga uchumi jumuishi na shindani unaowezesha ushiriki mpana wa wanawake katika maendeleo ya kiuchumi.