Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania

TanTrade Fostering Business

TANTRADE YASHIRIKI UFUNGUZI WA MAONESHO YA 5 YA KONGAMANO LA AFYA NA VIFAA TIBA

  • August 19, 2026


Dar es Salaam, 
19 Agosti 2026

Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) imeshiriki katika ufunguzi wa Maonesho ya 5 ya Kongamano la Afya na Vifaa Tiba, yanayofanyika kuanzia tarehe 19 hadi 21 Agosti 2026 katika ukumbi wa Diamond Jubilee Hall, Dar es Salaam.

Ushiriki wa TanTrade katika maonesho hayo unalenga kutoa fursa kwa wafanyabiashara, wazalishaji, wadau wa sekta mbalimbali na wananchi kufahamu huduma zinazotolewa na Mamlaka katika kukuza biashara za Tanzania, kutafuta masoko ya bidhaa za ndani, pamoja na kuwaunganisha wafanyabiashara na fursa za biashara katika masoko ya ndani na nje ya nchi.

Aidha, kupitia maonesho hayo, TanTrade inaendelea kuhamasisha matumizi ya Nembo ya Taifa ya “Made in Tanzania”, sambamba na kutoa elimu kwa wazalishaji na wafanyabiashara kuhusu umuhimu wa kuongeza ubora, ushindani na thamani ya bidhaa zinazozalishwa nchini ili ziweze kukidhi mahitaji ya masoko ya ndani na ya kimataifa.

Maonesho hayo pia yanatoa jukwaa kwa TanTrade kuendelea kujenga uhusiano na wadau wa sekta ya afya na viwanda, kubadilishana uzoefu, kutengeneza mitandao ya kibiashara na kutambua fursa mpya za biashara na ushirikiano.

TanTrade inawakaribisha wananchi, wafanyabiashara na wadau wa sekta mbalimbali hususan sekta ya vifaa tiba na vifaa vya Umeme kutembelea banda la TanTrade katika ukumbi wa Diamond Jubilee Hall, ili kupata elimu kuhusu huduma, fursa na programu mbalimbali zinazolenga kukuza biashara, masoko na bidhaa zinazozalishwa nchini.