TANTRADE YASHIRIKI KILELE CHA MAONESHO YA 3 YA FAHARI YA ZANZIBAR
- September 16, 2026
Zanzibar, 13 Septemba 2026
Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) imeshiriki katika hafla ya ufungaji rasmi wa Maonesho ya 9 ya Fahari ya Zanzibar, yaliyofanyika Zanzibar, ambapo mgeni rasmi alikuwa Mheshimiwa Shabani Ali Othuman, Waziri wa Vijana, Ajira na Uwezeshaji.
Akizungumza katika hafla hiyo, Naibu Mkurugenzi wa TanTrade, Ndugu Freddy Liundi, amepongeza ushirikiano uliowezesha kufanikisha maonesho hayo, akieleza kuwa ushiriki wa TanTrade ni sehemu ya jitihada za Mamlaka katika kukuza biashara, kutafuta na kuunganisha wafanyabiashara na masoko, pamoja na kutoa elimu kwa wazalishaji kuhusu fursa mbalimbali za kibiashara.
Ndugu Liundi pia amesisitiza umuhimu wa Nembo ya Made in Tanzania katika kutambulisha bidhaa zinazozalishwa nchini, kuongeza uaminifu wa watumiaji, kuimarisha ushindani wa bidhaa za Tanzania na kuwezesha bidhaa hizo kufikia masoko ya ndani na kimataifa.
Kwa upande wake, Waziri wa Vijana, Ajira na Uwezeshaji, Mheshimiwa Shabani Ali Othuman, ametoa maelekezo mbalimbali yenye lengo la kuongeza uzalishaji na tija, pamoja na kuboresha upatikanaji wa masoko kwa wafanyabiashara na wazalishaji.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusu fursa za biashara na uwekezaji, hususan namna ya kutumia fursa zilizopo katika masoko ya ndani na nje ya nchi ili kuongeza manufaa ya kiuchumi kwa wananchi.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Zanzibar (ZEEA), Ndugu Juma Burhan Mohammed, ameipongeza TanTrade kwa ushiriki wake wa kikamilifu katika kufanikisha maonesho hayo.
Amesema ZEEA itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha maonesho yajayo yanafanyika kwa mafanikio zaidi, huku ikisisitiza umuhimu wa kuongeza elimu na uelewa kwa wafanyabiashara na wazalishaji kuhusu fursa zilizopo za kukuza biashara na kuchangia maendeleo ya uchumi wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.
Katika maonesho hayo, TanTrade ilishiriki kikamilifu kwa kutoa elimu na taarifa mbalimbali kwa wananchi, wafanyabiashara na wazalishaji kutoka sekta tofauti, ikiwemo Kilimo na Uvuvi.
Kupitia banda lake, TanTrade pia iliwafikia wananchi mbalimbali kwa kuwajengea uelewa kuhusu majukumu yake, ikiwemo utoaji wa vibali vya kushiriki katika maonesho, pamoja na umuhimu wa Nembo ya Made in Tanzania katika kutambulisha bidhaa zinazozalishwa nchini.
Elimu hiyo imelenga pia kuwafahamisha wazalishaji namna Rajamu ya Taifa ya Made in Tanzania inavyoweza kuongeza uaminifu kwa watumiaji, kuimarisha ushindani wa bidhaa za Tanzania na kutoa fursa kwa bidhaa hizo kufikia masoko ya ndani na kimataifa.