Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania

TanTrade Fostering Business

TANTRADE YASHIRIKI ZIARA YA WAZIRI MKUU KUIMARISHA BIASHARA NA UWEKEZAJI QATAR

  • September 28, 2026


Doha, Qatar, 27 Septemba, 2026

Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) imeshiriki ziara ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba, nchini Qatar, inayolenga kuimarisha uhusiano wa kiuchumi na kupanua fursa za biashara na uwekezaji kati ya nchi hizo mbili.

Katika ziara hiyo, Waziri Mkuu amesisitiza umuhimu wa kuishirikisha sekta binafsi katika utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya Tanzania, hususan kufikia azma ya kuwa na uchumi wenye thamani ya dola za Marekani trilioni moja ifikapo mwaka 2050.

Amesema Serikali pekee haiwezi kufanikisha azma hiyo bila ushiriki wa wawekezaji wa ndani na nje. Hivyo, Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya biashara na kuweka vivutio vya uwekezaji vitakavyosaidia kuvutia mitaji, kuongeza uzalishaji na kuchochea ukuaji wa uchumi.

Viongozi wa Tanzania na Qatar pia wamejadili fursa za biashara na uwekezaji zinazoweza kunufaisha nchi hizo, ikiwemo kutumia nafasi ya Tanzania katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), pamoja na ushiriki wa Qatar katika Baraza la Ushirikiano la Nchi za Ghuba (GCC), kupanua wigo wa masoko na ushirikiano wa kiuchumi.

Aidha, wamejadili umuhimu wa kuwakutanisha wafanyabiashara wa Tanzania na Qatar kupitia taasisi zao za uwakilishi ili kutambua maeneo ya ushirikiano wa kimkakati, kujenga mahusiano ya kibiashara na kufungua fursa mpya za uwekezaji.

Kwa upande wake, Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Kapinga, ameitaka TanTrade kuongeza juhudi za kutambua na kukuza fursa za Tanzania katika masoko ya kimataifa, zikiwemo biashara ya huduma na rasilimali watu. Amesisitiza umuhimu wa Mamlaka kushirikiana na wadau katika kuwaunganisha wafanyabiashara na watoa huduma wa Tanzania na masoko ya nje.

Mkurugenzi Mkuu wa TanTrade, Bw. Ephraim Balozi Mafuru, ni miongoni mwa wakuu wa taasisi walioshiriki katika ziara hiyo. Ushiriki wa TanTrade unaimarisha utekelezaji wa jukumu lake la kutambua fursa, kukuza biashara na kuwaunganisha wafanyabiashara, watoa huduma na wawekezaji wa Tanzania na masoko ya kimataifa, ikiwemo Qatar.