TANTRADE YAZINDUA USAJILI WA KIDIGITALI SABASABA 2026 – JUBILEI YA DHAHABU
- February 6, 2026
Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) imezindua maandalizi ya Jubilei ya Dhahabu ya 50 ya Maonesho ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DITF 2026), maarufu kama Sabasaba, sambamba na mfumo mpya wa kidijitali wa usajili wa washiriki. Hafla imefanyika katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere na kuhudhuriwa na wadau wa sekta mbalimbali.
Akiongea katika uzinduzi huo, Mkurugenzi Mkuu wa TanTrade, Dkt. Latifa Mohammed Khamis, amethibitisha kaulimbiu ya mwaka huu kuwa ni “Sabasaba – Fahari ya Tanzania” ikisindikizwa na kauli ndogo “Bidhaa za Tanzania Kimataifa zaidi” na “Huduma za Biashara Kidigitali zaidi”. Pamoja na mambo mengine, amefafanua kuwa maandalizi hayo yamejikita katika teknolojia na maboresho ya huduma, ikiwemo mfumo wa usajili mtandaoni unaowawezesha washiriki kujisajili, kuomba maeneo, kupata vitambulisho, kulipia na kupata taarifa muhimu bila kufika ofisini.
Uzinduzi huu unaashiria mageuzi ya kidijitali sambamba na maadhimisho ya nusu karne ya maonesho makubwa ya biashara nchini Tanzania.