Julai 2026 - Mkoa wa Pwani.
Watumishi wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) wakiongozwa na Mkurugenzi Mkuu, Bw. Ephraim Balozi Mafuru, tarehe 31 Julai 2026 walifanya kikao kazi na Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhe. Abubakar Kunenge, katika ofisi yake mkoani humo. Lengo kuu lilikuwa kujadili na kuchambua fursa za biashara na uwekezaji zinazopatikana katika Mkoa wa Pwani, hususan maeneo yenye uwezo wa kutumika kwa shughuli za maonesho na biashara.
Katika majadiliano hayo, Mhe. Kunenge alieleza kwa kina fursa za kiuchumi zilizopo mkoani Pwani, akibainisha uwepo wa maeneo yanayoweza kuendelezwa kwa shughuli za biashara na uwekezaji. Alisisitiza umuhimu wa TanTrade kupata eneo maalum kwa ajili ya kuanzisha kituo kikubwa cha maonesho kitakachochochea biashara, uwekezaji na utalii wa kibiashara, na hivyo kuongeza mchango wa mkoa katika uchumi wa taifa.
Kwa upande wake, Bw. Mafuru alitoa shukrani kwa mapokezi mazuri na kuonesha utayari wa TanTrade kushirikiana na uongozi wa Mkoa wa Pwani katika kutambua na kuendeleza maeneo yanayofaa kwa shughuli za maonesho. Alisisitiza kuwa TanTrade itaendelea kutekeleza jukumu lake la kutafuta masoko ya bidhaa za kilimo na viwanda ndani na nje ya nchi, sambamba na kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kimataifa ili kuhakikisha wazalishaji wa Tanzania wanapata fursa pana za kibiashara.
Kikao kazi hiki kimeweka msingi wa ushirikiano wa kimkakati kati ya TanTrade na Mkoa wa Pwani, kwa lengo la kuendeleza fursa za biashara, kuvutia uwekezaji na kuimarisha nafasi ya Tanzania katika masoko ya kikanda na ya kimataifa. Mazungumzo haya yamefungua ukurasa mpya wa ushirikiano wa kimaendeleo, ambapo hatua za utekelezaji zitafuatilia makubaliano yaliyofikiwa ili kuhakikisha mkoa unakuwa kitovu cha biashara na maonesho ya kitaifa na kimataifa.