TANTRADE YAANGAZIA FURSA ZA BIASHARA KWA VIJANA KATIKA TANZANIA STARTUP WEEK 2026
- October 22, 2026
21 Oktoba 2026, Dar es Salaam
Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) imeangazia fursa za kuwawezesha vijana wajasiriamali kukuza biashara zao kupitia taarifa za masoko, kuwaunganisha na wanunuzi na wawekezaji, pamoja na ushiriki katika maonesho ya biashara ya ndani na nje ya nchi.
Huduma hizo zimeelezwa wakati wa ziara ya Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dennis Londo (Mb), aliyeambatana na Balozi wa Marekani nchini Tanzania, Mhe. William Trachman, katika banda la Wizara ya Viwanda na Biashara kwenye Kongamano la Wiki ya Biashara Bunifu Tanzania (Tanzania Startup Week 2026). Kongamano hilo linafanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaam, kuanzia tarehe 19 hadi 23 Oktoba 2026.
Katika ziara hiyo, Mhe. Londo amesisitiza kuwa ubunifu wa vijana ni nguzo muhimu katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050. Ameeleza kuwa uzoefu wa Marekani katika kuendeleza kampuni bunifu unaweza kuchangia ukuaji wa biashara changa nchini. Kwa upande wake, Balozi Trachman ameangazia umuhimu wa jukwaa hilo katika kuwaunganisha vijana wa Tanzania na kampuni za Marekani ili kuendeleza ubunifu, kupanua biashara na kunufaika na fursa za uwekezaji.
Kupitia ushiriki wake, TanTrade inawahamasisha wajasiriamali kuongeza thamani ya bidhaa zao, kutumia nembo ya “Made in Tanzania” na kuchangamkia fursa za masoko ya ndani na kimataifa. Juhudi hizo, pamoja na ushirikiano katika uwekezaji na uhamishaji wa teknolojia, zinalenga kuwawezesha vijana kubadilisha mawazo bunifu kuwa bidhaa na huduma zinazokidhi mahitaji ya soko na kujenga biashara zenye ushindani na uwezo wa kukua.