Akizungumza katika kikao cha Wizara ya Viwanda na Biashara kilichohusisha wadau wa sekta ya vinywaji vikali, Mkurugenzi Mkuu alisisitiza kuwa TanTrade itaendelea kulinda maslahi ya wazalishaji wa ndani, kuweka usimamizi rafiki za biashara, na kuhakikisha bidhaa za Tanzania zinapata nafasi pana katika masoko ya kimataifa.
Aidha, aliwataka wafanyabiashara kuwa na imani thabiti na ujasiri kwa TanTrade, akibainisha kuwa juhudi za kuimarisha mifumo ya biashara na uwekezaji zitawawezesha wazalishaji wa ndani kufikia masoko ya nje, kuongeza thamani ya bidhaa za Tanzania, na kuimarisha ajira na mapato ya taifa.
Mkurugenzi Mkuu pia alisisitiza kuwa TanTrade ni mali ya wafanyabiashara wa Tanzania, hivyo muda umefika kwa wadau wote kutoa ushirikiano wa karibu na taasisi hiyo. Ushirikiano huo utahakikisha TanTrade inatekeleza majukumu yake kwa ufanisi, ikiwemo kuratibu shughuli zote za biashara, kutatua changamoto za sekta, na kuunganisha wazalishaji na masoko ya kikanda na kimataifa.
Kwa ujumla, TanTrade imeandaa mfumo wa Made in Tanzania Logo, ambao unalenga kusaidia wazalishaji wa Tanzania kufikia masoko ya kimataifa kwa urahisi. Mfumo huo utasaidia kuwaunganisha wateja na wazalishaji wa bidhaa mbalimbali, hivyo kuongeza mwonekano na ushindani wa bidhaa za Tanzania katika anga za kimataifa.
Hata hivyo, bidhaa za Tanzania zimeendelea kushinda tuzo za ubora katika majukwaa ya kimataifa kila mwaka, jambo linalodhihirisha hadhi na ubora wa bidhaa za ndani na kuimarisha taswira ya Tanzania kama kitovu cha bidhaa bora na zenye viwango vya kimataifa.