TANTRADE YAWEKA MKAZO MATUMIZI YA BIDHAA ZA NDANI KATIKA UJENZI
- September 23, 2026
23 Septemba, 2026, Dar es salaam.
Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) imeendelea kuhamasisha matumizi ya bidhaa zinazozalishwa nchini katika sekta ya ujenzi, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kukuza viwanda vya ndani na kuongeza fursa za soko kwa wazalishaji wa Tanzania. Hayo yameelezwa wakati wa Maonesho ya 27 ya Kimataifa ya Ujenzi (Buildexpo Tanzania 2026), yaliyozinduliwa leo katika Kituo cha Maonesho cha Diamond Jubilee jijini Dar es Salaam.
Akizungumza katika maonesho hayo, Meneja wa Ukuzaji Biashara wa TanTrade, Bw. Deo Shayo, ametoa wito kwa waendelezaji wa majengo, wakandarasi na wazalishaji wanaoshiriki katika maonesho hayo kutoa kipaumbele kwa matumizi ya bidhaa na malighafi zinazozalishwa nchini katika miradi ya ujenzi na miundombinu.
Meneja Shayo amesema matumizi ya bidhaa za ndani, ikiwemo nondo, saruji na mbao, yana mchango katika kukuza viwanda vya ndani, kuongeza mzunguko wa fedha katika uchumi na kupunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje. Amesema sekta ya ujenzi ina nafasi kubwa katika kuunganisha uzalishaji wa ndani na mahitaji makubwa ya miundombinu yanayoendelea kuongezeka nchini.
Ameeleza kuwa ongezeko la watu na kasi ya ukuaji wa miji vinaendelea kuongeza mahitaji ya makazi nchini, huku takwimu zikionesha kuwa Tanzania inakabiliwa na upungufu wa nyumba unaokadiriwa kufikia milioni 3 na mahitaji ya takribani nyumba 200,000 kwa mwaka. Hali hiyo, amesema, inaonesha ukubwa wa soko na nafasi iliyopo kwa wazalishaji wa ndani kushiriki katika mnyororo wa thamani wa sekta ya ujenzi.
Kupitia utoaji wa vibali vya kielektroniki (ePermit) kwa maonesho ya biashara na kuwezesha majukwaa ya kimataifa kama Buildexpo Tanzania, TanTrade inaendelea kuwaunganisha wazalishaji wa ndani na wafanyabiashara, wawekezaji na wanunuzi kutoka ndani na nje ya nchi. Hatua hiyo inalenga kuongeza matumizi ya bidhaa za ndani na kuchochea uzalishaji, biashara, ajira na ukuaji wa uchumi nchini.