Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania

TanTrade Fostering Business

MKURUGENZI MKUU TANTRADE ATEMBELEA EACLC NA ENEO LA DUKA LA “MADE IN TANZANIA”

  • September 20, 2026


17 Septemba, 2026, Ubungo, Dar es Salaam

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade), Ephraim Balozi Mafuru, ametembelea Kituo cha Biashara cha Afrika Mashariki (EACLC) kilichopo Ubungo, Dar es Salaam, na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mkuu wa Kituo hicho, Bi. Catherine Wang.

Ziara hiyo ni ya kwanza kwa Mkurugenzi Mkuu Mafuru katika kituo hicho tangu ateuliwe kuiongoza TanTrade. Pamoja na kujitambulisha na kuimarisha uhusiano wa kikazi, viongozi hao wamejadili namna ya kuendeleza ushirikiano katika maeneo mbalimbali ya biashara na kufungua fursa zaidi kwa bidhaa zinazozalishwa nchini.

Aidha, Mafuru ametembelea eneo jipya lililotengwa kwa ajili ya kuanzishwa kwa duka maalumu la bidhaa za *“Made in Tanzania.”* Duka hilo linatarajiwa kutoa jukwaa la kudumu la kutangaza, kuonesha na kuuza bidhaa za Tanzania, hivyo kuwawezesha wazalishaji na wafanyabiashara kufikia wateja wengi zaidi na kupanua masoko yao.

Mafuru ameushukuru uongozi wa EACLC kwa mapokezi na jitihada zake za kukuza biashara, huku akieleza kuwa eneo la kimkakati la kituo hicho linatoa fursa muhimu kwa ukuaji wa biashara na upatikanaji wa masoko. Amewahimiza wajasiriamali na wafanyabiashara kuchangamkia fursa hiyo kwa kuchukua nafasi za ofisi katika EACLC na kutumia huduma zinazopatikana kituoni hapo kupanua shughuli zao. Ameahidi kuwa TanTrade itaendelea kushirikiana na uongozi wa EACLC ili kuhakikisha fursa zilizopo zinawanufaisha wazalishaji, wafanyabiashara na uchumi wa Taifa.