MKURUGENZI MKUU WA TANTRADE AFANYA ZIARA YA KIKAZI DODOMA
- August 7, 2026
Dodoma, 7 Agosti 2026
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade), Bw. Ephraim Balozi Mafuru, leo amefanya ziara ya kikazi katika Ofisi ya Kanda ya Kati, Dodoma. Katika ziara hiyo, Bw. Mafuru alikutana na watumishi wa Kanda inayohudumia mikoa ya Dodoma, Singida na Tabora, ambapo alifanya kikao cha kazi na kukagua mali za Taasisi zilizopo katika Mkoa wa Dodoma.
Akizungumza na watumishi, Mafuru alisisitiza umuhimu wa kuwajengea uwezo wafanyabiashara na wazalishaji wa bidhaa za Kitanzania ili kuongeza tija, thamani ya bidhaa na ushindani katika masoko ya ndani na nje ya nchi. Alibainisha kuwa TanTrade itaendelea kuimarisha jitihada za kuwaunganisha wazalishaji na masoko pamoja na kuvutia uwekezaji katika sekta za uchakataji wa mazao na bidhaa za mifugo.
Katika kikao hicho, Mkurugenzi Mkuu aliwaelekeza watumishi kuweka kipaumbele katika kutambua na kuendeleza fursa za biashara na uwekezaji zilizopo katika Mkoa wa Dodoma, hususan kwenye mazao na sekta zenye mchango mkubwa katika uchumi wa kanda hiyo.
Mafuru alisisitiza kuwa Mkoa wa Dodoma unaendelea kuwa kitovu cha uzalishaji wa zabibu nchini. Alitolea mfano kiwanda cha Swahili Honey kinachozalisha zaidi ya tani 650 kwa mwaka, huku akibainisha fursa kubwa za kuongeza thamani kupitia uchakataji wa juisi, mvinyo, zabibu kavu na bidhaa nyingine. Aliwataka watumishi kuendelea kukusanya na kuchambua taarifa za masoko, kuwaunganisha wakulima na viwanda vya uchakataji pamoja na kutafuta masoko mapya ya ndani na nje ya nchi.
Mafuru alieleza kuwa Dodoma ni miongoni mwa mikoa yenye idadi kubwa ya mifugo nchini, jambo linalotoa fursa kubwa katika biashara ya nyama, ngozi na bidhaa nyingine. Aliwaelekeza watumishi kuwatafutia wafugaji masoko ya uhakika, kuhamasisha uwekezaji katika viwanda vya kuchakata nyama na kuongeza thamani ya bidhaa kabla ya kuuzwa ndani na nje ya nchi.
Akizungumzia sekta ya ufugaji nyuki, Mafuru alisema Dodoma ina mazingira bora ya uzalishaji wa asali yenye ubora wa kimataifa. Alibainisha kuwa takwimu za Serikali zinaonesha mauzo ya asali nje ya nchi yaliongezeka kutoka tani 951.6 mwaka 2024 hadi tani 1,596.8 mwaka 2025, ishara ya kuongezeka kwa mahitaji ya kimataifa. Alisisitiza umuhimu wa wazalishaji kuongeza uzalishaji, kuboresha ubora, ufungashaji na kuzingatia viwango vya kimataifa ili kunufaika zaidi na masoko ya nje.
Aidha, Mafuru alibainisha kuwa TanTrade kupitia Ofisi ya Kanda ya Kati itaendelea kuhamasisha biashara ya mazao mengine yanayozalishwa kwa wingi katika kanda hiyo, yakiwemo alizeti, karanga, mtama na mazao ya jamii ya mikunde, kwa lengo la kuongeza thamani, kupanua masoko na kuongeza mchango wake katika uchumi wa wakulima na Taifa kwa ujumla.
Akihitimisha ziara hiyo, Bw. Mafuru aliwataka watumishi wa TanTrade kuendelea kufanya kazi kwa bidii, ubunifu na weledi katika kutekeleza majukumu yao ili kuongeza ufanisi wa Taasisi na kuchangia ukuaji wa sekta ya biashara nchini.