TANTRADE YAUNGANISHA WADAU WA MADINI NA FURSA ZA BIASHARA MAONESHO YA GEITA
- September 27, 2026
27 Septemba, 2026
Geita
Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade), Bwa. Freddy Liundi, amesema Maonesho ya 9 ya Teknolojia ya Madini Geita ni jukwaa la kuwaunganisha wachimbaji na fursa za teknolojia, masoko na uwekezaji ili kuongeza thamani ya madini na ushiriki wa Watanzania katika mnyororo wa thamani.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa maonesho hayo, Bwa. Liundi amesema sekta ya madini ina nafasi kubwa katika uchumi wa Taifa. Kwa mujibu wa takwimu za Benki Kuu ya Tanzania alizozitaja, mauzo ya madini yalifikia Shilingi trilioni 7.78 hadi Juni 2026, huku sekta hiyo ikichangia kwa wastani asilimia 32 ya mauzo ya Tanzania nje ya nchi.
Bwa. Liundi alisisitiza kuwa Serikali inataka kuona madini yakifungua fursa zaidi, biashara zaidi, ajira zaidi na viwanda zaidi kwa Watanzania,”.
Amesema TanTrade, kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Geita na Halmashauri ya Manispaa ya Geita, inatumia maonesho hayo kuwaunganisha wachimbaji, wafanyabiashara, wawekezaji, wanunuzi na wazalishaji wa teknolojia za uchimbaji na uongezaji thamani.
Katika banda lake, TanTrade imeweka Dawati la Usaidizi Wezeshi linalowakutanisha wadau na taasisi zikiwemo TRA, GS1, BRELA, Ofisi ya Mkemia Mkuu, STAMICO na FCC. Kupitia dawati hilo, wadau wanaweza kupata huduma na ufumbuzi wa changamoto zinazohusiana na biashara katika sekta ya madini. Maonesho hayo yanaendelea katika Viwanja vya Dkt. Samia Suluhu Hassan hadi tarehe 3 Oktoba 2026.