TANTRADE YATOA SEMINA MAALUM KUELEKEA SABASABA 50
- June 26, 2026
Dar es Salaam, 26 Juni 2026
Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE), kwa kushirikiana na wataalamu kutoka taasisi mbalimbali za usalama, afya na zimamoto, imeendesha semina maalum kwa washiriki wa Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba). Semina hii ni sehemu ya maandalizi ya maonesho ya Jubilei ya Dhahabu, ikilenga kuwajengea wadau uelewa wa kina kuhusu taratibu za usalama, afya na tahadhari za zimamoto wakati wa kipindi cha maonesho.
Semina imefanyika katika Ukumbi wa Rashidi Mfaume Kawawa Ceremonial Hall (DOME), uliopo ndani ya Viwanja vya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, jijini Dar es Salaam, na imekusanya wadau kutoka sekta mbalimbali. Lengo kuu lilikuwa kuhakikisha washiriki wanapata maarifa ya kitaalamu yatakayowawezesha kushiriki kwa usalama na ufanisi katika maonesho haya ya kihistoria.
Akifungua semina hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa TANTRADE, Dkt. Latifa Mohamed Khamis, aliwakaribisha washiriki na kutoa maelezo ya kina kuhusu maandalizi ya maonesho ya mwaka huu. Alisisitiza kuwa maadhimisho ya miaka 50 ya Sabasaba yameandaliwa kwa upekee, yakihusisha matukio maalum kama Usiku wa Miaka 50, ambapo wadau na washiriki waliotoa mchango mkubwa katika maendeleo ya maonesho kwa kipindi cha nusu karne watatunukiwa tuzo maalum.
Dkt. Khamis alieleza kuwa semina hii ni kielelezo cha dhamira ya TANTRADE kuhakikisha usalama na ustawi wa washiriki na wageni wote. Aliongeza kuwa maandalizi ya kisasa yamefanyika, ikiwemo maboresho ya miundombinu, usimamizi wa mabanda ya maonesho, na matumizi ya mfumo wa tiketi za kielektroniki ili kurahisisha uingiaji wa wageni na kuongeza ufanisi wa usimamizi.