TANTRADE YATANGAZA KUKAMIKA KWA MAANDALIZI KAMILI YA MAONESHO YA 50 YA DITF
Dar es Salaam - 24 June 2026
Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) imetangaza kukamilika kwa maandalizi ya Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DITF), maarufu Sabasaba, ambayo mwaka huu yanatarajiwa kuwa ya kipekee na yenye mvuto wa kipekee kutokana na programu mbalimbali maalum zitakazoratibiwa kwa washiriki wa ndani na nje ya nchi.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Juni 24, 2026 jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa TanTrade, Dk. Latifa Mohamed Khamis, alisema maonesho hayo yatafanyika kuanzia Juni 28 hadi Julai 13, 2026, yakilenga kuwakutanisha wafanyabiashara wa ndani na nje ya nchi ili kukuza biashara, uwekezaji na ubadilishanaji wa fursa za kiuchumi. Amesisitiza kuwa TanTrade kwa niaba ya Wizara ya Viwanda na Biashara imeendelea kushirikiana kwa karibu na sekta binafsi, ikiwemo jumuiya za wafanyabiashara, TCCIA, TPSF, wafanyabiashara wa Kariakoo pamoja na wadau wengine, ili kuhakikisha maonesho haya yanakuwa na manufaa makubwa kwa washiriki na taifa kwa ujumla.
Aidha, Dk. Latifa alibainisha kuwa moja ya vivutio vikubwa vya mwaka huu ni Usiku wa Jubilei ya Dhahabu utakaofanyika Julai 6, ambapo kutakuwa na maonesho ya kumbukumbu za kihistoria za Sabasaba kupitia filamu maalum ya kumbukumbu, utoaji wa tuzo kwa wadau waliotoa mchango mkubwa katika ukuaji wa maonesho hayo pamoja na sekta ya biashara kwa ujumla. Aliongeza kuwa waandishi wa habari nao watatambuliwa kwa mchango wao wa kipekee katika kutangaza maonesho haya kwa miaka yote, jambo litakaloongeza hadhi na heshima ya tasnia ya habari nchini.
Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuyaimarisha maonesho ya Sabasaba na kuyapa hadhi ya kimataifa, hali iliyochangia kuongezeka kwa ushiriki wa wafanyabiashara na wawekezaji kutoka mataifa mbalimbali. Hadi sasa, nchi 23 zimethibitisha ushiriki wao, huku matarajio yakiwa ni kuongezeka zaidi kutokana na maandalizi yanayoendelea katika nchi nyingine ikiwemo Burundi, Kenya na Algeria. Ushiriki huu wa kimataifa unadhihirisha nafasi ya Tanzania kama kitovu cha biashara na uwekezaji katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
Dk. Latifa amewakaribisha Watanzania na wadau wa biashara kutoka ndani na nje ya nchi kushiriki kikamilifu katika maonesho haya ya kihistoria, akisisitiza kuwa yatatoa fursa muhimu za biashara, uwekezaji na ushirikiano wa kiuchumi. Ameongeza kuwa DITF ya mwaka huu itakuwa jukwaa la kuonyesha ubunifu wa Watanzania, kuhamasisha vijana kushiriki katika ujasiriamali, na kuimarisha nafasi ya Tanzania katika biashara za kimataifa.