TANTRADE NA TPSF ZAIMARISHA USHIRIKIANO NA MKOA WA MWANZA KATIKA KUKUZA BIASHARA NA UWEKEZAJI
- October 26, 2026
23 Oktoba 2026 , Mwanza
Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) imeendelea kuimarisha ushirikiano na Serikali za Mikoa pamoja na sekta binafsi ili kupanua fursa za biashara na uwekezaji. Katika kuendeleza juhudi hizo, Mkurugenzi Mkuu wa TanTrade, Ephraim Balozi Mafuru, ameshiriki mazungumzo na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. CP Salum Hamduni, pamoja na Afisa Mtendaji Mkuu wa Shirikisho la Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Bw. Deogratius Massawe.
Mazungumzo hayo yamejikita katika kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi, kutambua fursa za kiuchumi zilizopo mkoani Mwanza na kujenga mahusiano yatakayochochea biashara na uwekezaji. Kwa TanTrade, ushirikiano huo ni sehemu ya juhudi za kuwaunganisha wafanyabiashara na wadau wanaoweza kusaidia kupanua shughuli zao na kufikia masoko.
Jioni, Mhe. Hamduni anatarajiwa kuwa Mgeni Rasmi katika hafla ya chakula cha jioni iliyoandaliwa na TPSF katika Hoteli ya Malaika, jijini Mwanza. Hafla hiyo inalenga kuwakutanisha wadau wa biashara na uwekezaji ili kubadilishana mawazo, uzoefu na kutambua maeneo ya ushirikiano.
Ushiriki wa TanTrade katika mazungumzo hayo unaweka msisitizo katika umuhimu wa kuratibu juhudi za Serikali na sekta binafsi ili kuzigeuza fursa zilizopo mkoani Mwanza kuwa shughuli za biashara zenye tija kwa wafanyabiashara na uchumi wa Taifa.