TANTRADE YAWA MWAROBAINI WA CHANGAMOTO ZA WAFANYABIASHARA ZANZIBAR
- September 6, 2026
Zanzibar, 5 Septemba, 2026
Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) imeendelea kuwa mwarobaini wa changamoto zinazowakabili wafanyabiashara kwa kuwakutanisha katika eneo moja na taasisi mbalimbali zinazowezesha na kusimamia biashara kupitia Kliniki ya Biashara katika Tamasha la Tatu la Fahari ya Zanzibar.
Kliniki hiyo inawakutanisha wafanyabiashara na taasisi mbalimbali, zikiwemo BPRA, ZRA, ZBS, ZNCC na ZEEA, ili kupata elimu, ushauri na ufumbuzi wa moja kwa moja kuhusu masuala ya usajili wa biashara, kodi, viwango na ubora wa bidhaa, pamoja na fursa za uwezeshaji na maendeleo ya biashara.
Kupitia huduma hiyo, TanTrade inarahisisha upatikanaji wa taarifa na huduma muhimu kwa wafanyabiashara, huku ikiwaunganisha na fursa za masoko ya ndani na nje ya nchi. Hatua hii inalenga kupunguza changamoto zinazoweza kukwamisha ukuaji wa biashara na kuwawezesha wafanyabiashara kuongeza ushindani wa bidhaa na huduma zao.
Aidha, katika eneo hilo wafanyabiashara wanapatiwa elimu kuhusu umuhimu wa utambulisho wa bidhaa zinazozalishwa nchini pamoja na huduma za usajili wa Nembo za “Made in Tanzania” na “Made in Zanzibar.” Nembo hizo zinasaidia kujenga utambulisho, kuongeza uaminifu wa bidhaa na kuimarisha ushindani wake katika masoko ya ndani na kimataifa.
Mkurugenzi Mkuu wa TanTrade, Bw. Ephraim Balozi Mafuru, ametembelea Banda la TanTrade na eneo la Kliniki ya Biashara kujionea huduma zinazotolewa kwa wafanyabiashara wanaoshiriki na kutembelea Tamasha hilo.
Ushiriki wa TanTrade katika Fahari ya Zanzibar 2026 unaendeleza dhamira ya Mamlaka ya kusogeza huduma karibu na wafanyabiashara, kutatua changamoto zao na kujenga mazingira yatakayowezesha bidhaa zinazozalishwa nchini kupata masoko na kushindana kimataifa.