Tanzania Yaendelea Kuimarisha Sekta ya Vinywaji Vikali kwa Viwango vya Kimataifa
- August 25, 2026
Dar es Salaam, 24 Agosti 2026
Serikali imekutana na wamiliki wa viwanda vinavyozalisha vinywaji vikali nchini kwa lengo la kujadili namna bora ya kuimarisha sekta hiyo na kuhakikisha bidhaa zinazozalishwa zinakidhi viwango vya ubora na usalama wa watumiaji.
Kikao hicho, kilichoongozwa na Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Kapinga (Mb.), kiliweka mkazo katika kujenga mazingira rafiki ya biashara, kulinda afya na usalama wa wananchi, na kuhakikisha ushindani wa haki katika soko. Waziri Kapinga alisisitiza kuwa sekta ya vinywaji vikali ni miongoni mwa sekta zenye mchango mkubwa katika uchumi wa taifa, ikitoa ajira kwa maelfu ya Watanzania, kuongeza mapato ya Serikali kupitia kodi na ushuru, na kuchangia ukuaji wa biashara ya ndani na ya kimataifa.
Katika maelezo yake, Mhe. Kapinga aliwahimiza wazalishaji kuendelea kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za uzalishaji, huku akisisitiza umuhimu wa kuhakikisha bidhaa zote zinakidhi viwango vya ubora vinavyosimamiwa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kabla ya kuingia sokoni. Alibainisha kuwa Serikali imejipanga kuhakikisha sekta ya vinywaji vikali inakuwa mfano wa kuigwa katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika kwa kuzalisha bidhaa salama, zenye ubora wa kimataifa na zinazokubalika katika masoko ya kikanda na ya dunia.
Aidha, Serikali imewahakikishia wadau kuwa itaendelea kushirikiana nao katika kuimarisha elimu kwa wafanyabiashara na wananchi kuhusu umuhimu wa kutumia vinywaji vilivyothibitishwa na TBS. Hatua hii inalenga kuongeza uelewa wa watumiaji, kuimarisha imani ya soko na kuhakikisha bidhaa zinazofika kwa wananchi ni salama na zenye ubora wa kimataifa.
Miongoni mwa washiriki wa kikao hicho alikuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania- TanTrade, Bw. Ephraim Balozi Mafuru, ambaye alisisitiza kuwa TanTrade itaendelea kushirikiana na Wizara, taasisi za udhibiti na sekta binafsi katika kuwezesha bidhaa halali na zenye ubora kufikia masoko ya ndani na nje ya nchi. Aliongeza kuwa TanTrade itahakikisha wafanyabiashara wanapata elimu ya biashara, fursa za mikutano ya kibiashara (B2B) na msaada wa kitaasisi ili kuimarisha ushindani wa haki na kuongeza thamani ya bidhaa za Tanzania.
Zaidi ya hayo, Serikali imehakikishia masoko ya kimataifa hususan katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kuwa bidhaa za vinywaji kutoka Tanzania ni bora na zenye viwango vya kimataifa. Bidhaa hizi zimekuwa zikishinda tuzo za ubora katika anga za kimataifa kila mwaka, jambo linalothibitisha ubora na ushindani wake katika soko la dunia. Ushindi huu wa mara kwa mara ni uthibitisho wa dhamira ya Tanzania ya kuendelea kuzalisha bidhaa bora zinazokidhi mahitaji ya watumiaji wa ndani na wa kimataifa.
Serikali imesisitiza kuwa mafanikio ya sekta ya vinywaji vikali yanategemea ushirikiano wa wadau wote, wakiwemo wazalishaji, wafanyabiashara na wananchi. Kupitia juhudi hizi, Tanzania imeweka bayana dhamira yake ya kuendelea kuzalisha vinywaji bora na salama, vinavyokidhi viwango vya kimataifa na kuimarisha nafasi ya nchi katika masoko ya kikanda na ya dunia.