Speech by Hon. Ambassador Dr. Emmanuel Nchimbi
- July 8, 2026
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
OFISI YA MAKAMU WA RAIS
HOTUBA YA MHE. BALOZI DKT. EMMANUEL NCHIMBI, MAKAMU WA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA KWENYE HAFLA YA KUSHEREHEKEA MIAKA 50 YA MAONESHO YA BIASHARA YA KIMATAIFA YA DAR ES SALAAM (DITF) DAR ES SALAAM 06 JULAI 2026 •
Mhe. Judith Kapinga, Waziri wa Viwanda na Biashara; •
Mhe. Albert Chalamila, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam; •
Mhe. Denis Londo, Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara; •
Bw. Waziri Salum, Katibu Mkuu, Wizara ya Viwanda na Biashara, na Makatibu Wakuu wote mliohudhuria; •
Prof. Ulingeta Mbamba, Mwenyekiti wa Bodi, pamoja na Wajumbe wote wa Bodi ya TANTRADE; •
Dkt. Latifa Khamis, Mkurugenzi Mkuu wa TANTRADE; •
Waheshimiwa Mabalozi na Washirika wa Maendeleo mliopo; •
Viongozi wa Serikali na Sekta Binafsi; •
Menejimenti na Watumishi wa TANTRADE; •
Wafanyabiashara; •
Waandishi wa Habari; •
Wageni waalikwa; •
Mabibi na Mabwana.
Kazi na Utu....!
Kwanza kabisa, sina budi kumshukuru Mwenyezi Mungu aliyetuwezesha kushiriki hafla hii ya kihistoria ya miaka hamsini ya Maonesho ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DITF), maarufu kama ‘Sabasaba’, tukiwa wazima na wenye afya njema. Kabla sijaendelea, napenda kuleta kwenu salamu za Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambaye anawapongeza na kuwatakia Jubilei njema. Jubilei hii ni tukio la kihistoria lilonatupa fursa ya kutafakari na kusherehekea mafanikio yetu, na pia kujipanga kutekeleza dhamana yetu katika kipindi kijacho. Tukio hili linatupa fahari kwetu sisi sote tukiwa kama sekta binafsi, wazalishaji, wawekezaji na wananchi wote, hasa wanaoamini kuwa biashara na viwanda ni muhimu katika maendeleo ya Taifa. Waheshimiwa Viongozi na Ndugu Washiriki; Katika miaka hamsini iliyopita, tumeshuhudia Maonesho ya Sabasaba yakikua na kubadilika, ambapo yamekua zaidi ya maonesho ya biashara bali darasa la ujasiriamali, soko la bidhaa za Tanzania, jukwaa la ubunifu, na daraja linalounganisha wazalishaji wetu na masoko ya ndani na nje ya 1 nchi. Hivyo, Jubilei hii ya Dhahabu ni fursa adhimu kwetu ya kuangalia tuliko toka, tulipo na tunakoelekea ili kubainisha vikwazo na fursa zilizopo. Tangu tarehe 1 Julai, 2026, Tanzania imeanza rasmi kutekeleza rasmi Dira ya 2050, inayoweka msingi wa Tanzania kuwa Taifa lenye uchumi shindani, viwanda vya kisasa, biashara bunifu, wananchi wenye ujuzi na uchumi unaotegemea maarifa, teknolojia na ubunifu. Kwa msingi huo, Jubilei hii ya Dhahabu ituelekeze katika safari nyingine ya miaka hamsini itakayotoa mchango katika kuijenga Tanzania ya mwaka 2050. Waheshimiwa Viongozi na Ndugu Washiriki; Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imedhamiria kujenga uchumi shindani wa viwanda ili kuifikisha nchi yetu kwenye kipato cha kati cha juu. Ili kufikia azma hii, Serikali imeendelea kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara na uwekezaji kwa kiwango kikubwa. Mathalan, Serikali imeweka sera sahihi, imejenga miundombinu, imeimarisha taasisi na kuwezesha sekta binafsi kufanya biashara kwa ufanisi zaidi. Matokeo yake tunashuhudia viwanda vipya vinaendelea kujengwa, uzalishaji unaongezeka, ajira zinaongezeka na bidhaa za Tanzania zinaendelea kupata nafasi kubwa zaidi katika masoko ya kikanda na kimataifa. Waheshimiwa Viongozi na Ndugu Washiriki; Kama mnavyofahamu, katika siku za hivi karibuni, Nchi yetu imechukua hatua nyingine muhimu ya kuanzisha alama maalum ya bidhaa za Tanzania, yaani Made in Tanzania. Alama ambayo si ya biashara pekee bali heshima ya Taifa kwani inatambulisha ubora wa bidhaa zetu. Ninatoa wito kwa wazalishaji wote kuitumia ipasavyo alama hii ili kujenga hadhi ya bidhaa za Tanzania na kuongeza ushindani wake katika masoko ya Afrika na duniani. Waheshimiwa Viongozi na Ndugu Washiriki; Ili kutoa mchango stahiki katika utekelezaji wa Dira ya 2050, tunahitaji kufanya mabadiliko makubwa zaidi katika sekta ya viwanda na biashara. Ni lazima kufanya uzalishaji wa bidhaa zenye thamani kubwa, na kutumia teknolojia za kisasa katika uzalishaji. Ni muhimu pia kuongeza ubunifu ili 2 kuanzisha kampuni zitakazozalisha bidhaa zenye ubora na ushindani katika masoko. Aidha, masuala ya utafiti, ubunifu na matumizi ya akili unde (Artificial Intelligence), biashara za kidijitali na mifumo ya kisasa ni lazima viwe sehemu ya ukuaji wa uchumi wetu. Ifikapo mwaka 2050, tunataka DITF isiwe mahali pa kuonesha bidhaa pekee bali kitovu cha ubunifu, utafiti, teknolojia na biashara za kimataifa; mahali pa kuonesha zaidi teknolojia na bunifu mbalimbali; mahali pa kuunganisha wawekezaji na wabunifu; mahali zinapozinduliwa bidhaa mpya za Tanzania kwa soko la dunia; na, jukwaa la wafanya biashara wa Tanzania na Afrika. Waheshimiwa Viongozi na Ndugu Washiriki; Ili kukuza uzalishaji na kuimarisha sekta ya viwanda ni muhimu kushughulikia suala la upatikanaji wa mitaji. Serikali inatambua kuwa kumekuwa na changamoto kubwa ya upatikanaji wa mitaji kwa ajili ya kuanzisha na kuendeleza viwanda vidogo na vya kati. Hivyo, ni muhimu Taasisi za fedha zijielekeze zaidi katika kusaidia sekta hii, hususan viwanda vidogo vidogo kwa kuweka masharti ya mikopo ya upendeleo kwa viwanda vidogo na vya kati. Nazipongeza taasisi za fedha ambazo tayari zinatoa huduma hii kwani hatua hiyo imesaidia kupunguza vikwazo vinavyosababisha wajasiriamali wengi kushindwa kupata mikopo. Waheshimiwa Viongozi na Ndugu Washiriki; Nimefahamishwa kuwa katika hafla hii Tuzo za Jubilei ya Dhahabu zitatolewa kwa wafanyabiashara, wazalishaji na wadau mbalimbali ambao mchango wao umekuwa chachu katika maendeleo ya biashara nchini. Kwa kutumia fursa hii, nawapongeza wote mtakaotunukiwa tuzo hizo. Pamoja na kutunukiwa Tuzo, nawasihi kuendelea kuboresha na kuongeza uzalishaji ili kuendelea kutoa mchango katika kukuza uchumi. Tungependa kuona Tuzo hizi zinakuwa chachu ya ubunifu, ushindani, uwekezaji na uzalishaji wenye tija zaidi. Waheshimiwa Viongozi na Ndugu Washiriki; Napenda kuhitimisha hotuba yangu kwa kusisitiza umuhimu wa maonesho ya biashara katika ukuaji wa Uchumi. Katika kipindi cha miaka 50 iliyopita, Maonesho ya Sabasaba yametujengea msingi wa ushindani kibiashara, 3 yamechochea ukuaji wa biashara na kujenga uwezo wa wafanyabiashara na wazalishaji; na, kuimarisha uhusiano baina ya wazalishaji na walaji. Katika safari ya kuelekea mwaka 2050, ninaitaka DITF kuimarisha mchango wake kwa kuyafanya maonesho haya kuwa miongoni mwa maonesho makubwa zaidi ya biashara duniani, yakiiweka Tanzania kama kitovu cha biashara, uwekezaji, ubunifu na viwanda barani Afrika. Baada ya kusema hayo, naipongeza Bodi ya Biashara za Nje (BET) kwa kuandaa Jubilei hii ya Dhahabu, na nawashukuru nyote kwa kushiriki hafla hii na Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam. Mungu ibariki Tanzania. Asanteni sana kwa kunisikiliza.