Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania

TanTrade Fostering Business

SAMIALISM YAPONGEZA TANTRADE KWA UTUNZAJI MAZINGIRA

  • April 22, 2026

SAMIALISM YAPONGEZA TANTRADE KWA UTUNZAJI MAZINGIRA

22 Aprili, 2026
Dar Es Salaam
______________________________________________
Mkurugenzi Mkuu wa Tantrade, Dkt. Latifa Mohamed Khamis, amekutana na viongozi wa jukwaa la Samialism na kufanya mazungumzo ya kina kuhusu umuhimu wa kuhamasisha jamii juu ya utunzaji wa mazingira. Mazungumzo hayo yalijikita zaidi katika dhana ya kupanda miti ya vivuli na matunda, hatua inayolenga kuboresha hali ya hewa, kupunguza joto, na kuongeza rasilimali za chakula kwa vizazi vijavyo.

Katika kikao hicho, Tantrade ilipata nafasi ya kuwakaribisha wageni hao na kuwapeleka kutembelea viwanja vya maonesho ya Sabasaba. Wageni walipata fursa ya kushuhudia hali ya mazingira yanayozunguka eneo hilo, ikiwemo jitihada za kupendezesha mandhari, kupanda miti, na kuimarisha usafi wa mazingira. Ziara hiyo ililenga kuonesha kwa vitendo namna Tantrade inavyotekeleza wajibu wake wa kulinda mazingira na kuhamasisha wadau wengine kuiga mfano huo.

Akizungumza kwa niaba ya jukwaa la Samialism, Mwenyekiti Charles Wilbrad aliipongeza Tantrade kwa juhudi zake za dhati katika kulinda na kutunza mazingira. Alisisitiza kuwa juhudi hizo ni za kuigwa na taasisi nyingine, na akahimiza kuongeza nguvu katika kampeni za uhamasishaji wa utunzaji wa mazingira hususan ndani ya maeneo ya Sabasaba. Aidha, alieleza kuwa hatua za kupanda miti na kuendeleza mandhari safi ni msingi wa kujenga jamii yenye afya bora na mazingira endelevu.

Kwa upande wake, Dkt. Latifa Mohamed Khamis aliahidi kuwa Tantrade itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuhakikisha kuwa utunzaji wa mazingira unakuwa ajenda ya kudumu. Alisisitiza kuwa maonesho ya Sabasaba si tu jukwaa la biashara, bali pia ni kioo cha kuonesha wajibu wa kijamii katika kulinda mazingira na kuhamasisha vizazi vipya kuishi kwa kuzingatia misingi ya uendelevu.