Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania

TanTrade Fostering Business

MAANDALIZI YA SABASABA YA DHAHABU 2026 YAPAMBA MOTO

  • April 9, 2026

  
Dar es Salaam, 09 Aprili 2026

Maonesho ya Sabasaba 2026 yamewakutanisha wadau kujadili na kuweka mikakati madhubuti ya kuboresha maadhimisho ya Jubilei ya Dhahabu ya miaka 50 ya maonesho hayo.  

Katika kikao hicho, mawasilisho ya hatua za maandalizi yalijadiliwa kwa kina, yakilenga kuhakikisha maonesho ya mwaka 2026 yanafanyika kwa viwango vya juu vya ubora, ubunifu na ushindani, pamoja na kuvutia washiriki wengi zaidi kutoka ndani na nje ya nchi.  

Akiongoza kikao hicho, Mwenyekiti ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Mhe. Balozi Waziri Rajab Salum, alieleza kuridhishwa na maendeleo yaliyofikiwa hadi sasa katika maandalizi ya maonesho hayo. Aidha, alisisitiza umuhimu wa ushirikishwaji mpana wa wadau mbalimbali, hususani vijana wafanyabiashara wabunifu na wachanga, pamoja na sekta zote za uzalishaji na huduma, ili kuchochea ukuaji wa uchumi wa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.  

Kikao hicho pia kilijadili masuala ya miundombinu ya maonesho, ushiriki wa kimataifa, na maboresho ya huduma kwa washiriki na wageni, ikiwemo matumizi ya teknolojia za kidigitali katika usajili na uratibu wa shughuli. Wadau walitoa mapendekezo kuhusu namna bora ya kuimarisha mazingira ya biashara, kuongeza fursa za mawasiliano ya moja kwa moja kati ya wazalishaji na wanunuzi, na kuendeleza ubunifu wa bidhaa za ndani ili ziweze kushindana katika masoko ya kikanda na kimataifa.  

Zaidi ya hayo, kikao kilisisitiza umuhimu wa kushirikiana na taasisi wezeshi kupitia *Business Clinic*, ili kurahisisha huduma kwa wafanyabiashara na kuhakikisha maonesho yanakuwa jukwaa la kutoa suluhisho la changamoto za sekta binafsi. Ushirikiano huu unatarajiwa kuongeza ufanisi wa maonesho na kuimarisha taswira ya Tanzania kama kitovu cha biashara Afrika Mashariki na Kati.  

Kwa ujumla, maandalizi ya Sabasaba ya Dhahabu 2026 yamepamba moto, yakionesha dhamira ya dhati ya Serikali na wadau wa sekta binafsi kuhakikisha maadhimisho haya ya miaka 50 yanakuwa ya kihistoria, yenye mvuto wa kimataifa na mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa taifa.