Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania

TanTrade Fostering Business

KAMATI YA MAANDALIZI YA MAONESHO SABASABA 2026 YAKUTANA

  • April 2, 2026


Dar es Salaam, 01 Aprili 2026

Kamati ya Maandalizi ya Maonesho ya Sabasaba 2026 imekutana katika makao makuu ya TanTrade kujadili mikakati ya kuboresha mchakato wa maandalizi ya maadhimisho ya miaka 50 ya SABASABA 2026.
Katika kikao hicho, Mkurugenzi wa TanTrade, Dkt. Latifa Khamis, aliwasilisha mkakati wa awali wa maandalizi, ukilenga kuhakikisha maonesho ya mwaka 2026 yanatekelezwa kwa viwango vya juu vya ubora na kuvutia washiriki wengi zaidi kutoka ndani na nje ya nchi.

Baada ya mawasilisho hayo, Mwenyekiti wa kikao, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Bw. Aristides Robert Mbwasi, aliridhishwa na hatua zilizofikiwa katika maandalizi ya maonesho. Aidha, alisisitiza umuhimu wa kuongeza kasi ya utekelezaji kwa kuwa maonesho haya ni ya kihistoria na yana nafasi kubwa katika kuchochea maendeleo ya biashara na uchumi wa taifa.

Vilevile, wajumbe wa kamati walijadili masuala ya ushirikishwaji wa wadau mbalimbali, ikiwemo sekta binafsi, mashirika ya kimataifa, na washirika wa maendeleo, ili kuhakikisha maonesho ya mwaka huu yanakuwa jukwaa la kimataifa la biashara na uwekezaji. Pia walisisitiza umuhimu wa kuimarisha kampeni za uhamasishaji ndani na nje ya nchi, hususan kupitia vyombo vya habari na majukwaa ya kidigitali, ili kuongeza idadi ya washiriki na wageni wa kimataifa.

Kamati ilikubaliana pia kuimarisha maandalizi ya maonesho kwa kuzingatia vipengele vya ubunifu, teknolojia, na urithi wa kitamaduni wa Tanzania, ili kuonyesha sura halisi ya maendeleo ya viwanda na biashara kwa kipindi cha nusu karne.
Kwa pamoja, wajumbe walitoa wito wa mshikamano na mshirikiano wa kitaifa katika kuhakikisha maonesho ya SABASABA 2026 yanakuwa ya kipekee, yenye tija, na yanayoacha alama ya kudumu katika historia ya taifa.