MAANDALIZI YA MAONESHO YA SABASABA 50 YAPEWA KIPAUMBELE NA VIONGOZI
- May 14, 2026
Dar es Salaam, 14 Mei 2026
Katibu Mkuu wa Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda Zanzibar, Dkt. Habiba Hassan Omar, amefanya ziara katika Ofisi za Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) na kukagua maandalizi ya Maonesho ya Jubilei ya Miaka 50 ya Biashara ya Kimataifa Dar es Salaam (Sabasaba). Katika ziara hiyo, Dkt. Habiba alieleza kuridhishwa kwake na hatua zilizofikiwa hadi sasa na kusisitiza umuhimu wa ushiriki wa wadau katika maonesho hayo makubwa ya kihistoria.
Aidha, Dkt. Habiba alipata nafasi ya kuzungumza na Kamati ya Kitaifa ya Ulinzi na Usalama, ambayo inaratibu masuala ya kiusalama wakati wa kipindi chote cha maonesho. Mazungumzo hayo yalilenga kuhakikisha maandalizi ya Sabasaba yanakwenda sambamba na viwango vya usalama wa kitaifa, huku ikisisitizwa kuwa usalama wa wageni na washiriki ni kipaumbele cha juu.
Kwa upande wa TanTrade, Mkurugenzi Mkuu Dkt. Latifa M. Khamis alieleza hatua zilizofikiwa katika maandalizi, ikiwemo uandaaji wa maeneo ya maonyesho, maboresho ya miundombinu, na maandalizi ya programu maalum zitakazofanyika wakati wa maonesho. Programu hizo zinajumuisha mikutano ya B2B, kongamano la kimataifa, siku za kitaifa, tuzo za biashara, pamoja na maonesho ya utamaduni na burudani. Dkt. Latifa alisisitiza kuwa maonesho ya mwaka huu yatakuwa na upekee wa kipekee, yakidhihirisha historia ya nusu karne ya Sabasaba na mchango wake katika kukuza biashara na uwekezaji.
Maonesho haya yanatarajiwa kufanyika kuanzia tarehe 28 Juni hadi 13 Julai 2025 katika Uwanja wa Maonesho wa Mwalimu J.K. Nyerere, Barabara ya Kilwa, Dar es Salaam, yakihusisha zaidi ya nchi 50 na makampuni makubwa ya ndani na nje ya nchi. Hii ni fursa ya kipekee kwa Tanzania kuonesha bidhaa na huduma zake, kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kimataifa, na kuendeleza taswira ya taifa katika majukwaa ya biashara duniani.