Mtwara, 10 Augusti 2026
Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Salvio Kapinga (Mb.), anaongoza ziara ya siku tatu mkoani Mtwara kuanzia tarehe 10 hadi 12 Agosti 2026, yenye mwelekeo wa kuimarisha biashara na kuongeza thamani ya mazao ya kilimo.
Ziara hii inalenga kuzindua na kuweka mawe ya msingi katika miradi ya kimkakati, huku ikisisitiza umuhimu wa kuimarisha minyororo ya thamani na kupanua masoko ya bidhaa za Tanzania. Katika ziara hiyo, Mhe. Waziri ameambatana na Ndg. Ephraim Balozi Mafuru, Mkurugenzi Mkuu wa TanTrade, pamoja na viongozi wengine wa Serikali na sekta binafsi, ambapo ushiriki wa TanTrade unasisitiza jukumu lake la kitaasisi katika kukuza biashara, kuendeleza mauzo ya nje na kuimarisha taswira ya bidhaa za Tanzania katika masoko ya kikanda na kimataifa.
Miradi inayotembelewa ni pamoja na Kiwanda Darasa cha Kubangua Korosho (KIDAKUKO) Mandiwa, ambacho kinatarajiwa kuongeza thamani ya korosho na kuimarisha nafasi ya Tanzania katika soko la dunia; Ghala la Kuhifadhia Mazao Mtandi, litakalopunguza upotevu wa mazao na kuongeza ufanisi wa usambazaji; miradi ya maji na ujenzi wa shule za msingi na sekondari; mabweni ya Shule ya Sekondari ya Wasichana Mtwara; pamoja na Kituo cha Afya Msangamkuu kitakachoboresha ustawi wa jamii na nguvu kazi yenye afya.
Mbali na uzinduzi wa miradi, ziara hii itatoa fursa kwa Mhe. Waziri kukutana na wafanyabiashara wa Mkoa wa Mtwara katika mkutano maalum jijini Mtwara. Mkutano huo utakuwa jukwaa la kujadili changamoto za biashara, fursa za kukuza mauzo ya nje hususan korosho na mazao mengine ya kilimo, pamoja na mikakati ya kuongeza thamani na kupanua masoko ya bidhaa za Mtwara.
Kwa ujumla, ziara hii ni hatua ya kimkakati inayolenga kuimarisha biashara na usafirishaji wa bidhaa za Tanzania. Kupitia miradi inayozinduliwa na majadiliano na wafanyabiashara, Serikali kwa kushirikiana na TanTrade inalenga kujenga mazingira bora ya biashara, kuongeza ajira na mapato ya wakulima, na kuimarisha ushindani wa bidhaa za Tanzania katika masoko ya kikanda na kimataifa.