Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania

TanTrade Fostering Business

WAZIRI KAPINGA ARIDHISHWA NA JUHUDI ZA TANTRADE KATIKA KUKUZA BIASHARA NA KUWEZESHA WAZALISHAJI WA NDANI

  • November 3, 2026

02 Novemba 2026 | Dodoma

Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Salvio Kapinga (Mb), ametembelea banda la Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) katika maonesho yanayofanyika kuelekea uzinduzi wa Sera ya Maendeleo Endelevu ya Viwanda na Sera ya Maendeleo ya Wajasiriamali Wadogo na wa Kati (SMEs). Maonesho hayo yanayoshirikisha Wizara ya Viwanda na Biashara, taasisi zilizo chini ya Wizara hiyo pamoja na wadau wa sekta binafsi, yanafanyika kuanzia tarehe 02 hadi 04 Novemba 2026 katika Kituo cha Mikutano cha Jakaya Kikwete (JKCC), jijini Dodoma.

Akiwa kwenye banda la TanTrade, Mhe. Kapinga alipata maelezo kuhusu majukumu na shughuli mbalimbali zinazotekelezwa na Mamlaka hiyo katika kukuza biashara nchini, kuimarisha ushindani wa bidhaa za Tanzania na kuwasaidia wafanyabiashara pamoja na wazalishaji kupata fursa za masoko ndani na nje ya nchi.

Akitoa maelezo kwa Waziri, maafisa wa TanTrade walieleza jinsi Mamlaka inavyotekeleza programu mbalimbali za kuwawezesha wafanyabiashara na wajasiriamali kupitia utoaji wa taarifa za masoko, uratibu wa ushiriki katika maonesho ya biashara ya ndani na kimataifa, pamoja na kuwaunganisha wazalishaji na wanunuzi kutoka masoko tofauti duniani.

Mhe. Kapinga pia alielezwa kuhusu juhudi zinazoendelea za TanTrade katika kutoa elimu kwa wazalishaji kuhusu taratibu za usajili na matumizi ya Nembo ya “Made in Tanzania”, ambayo imeanzishwa mahsusi kutambulisha bidhaa na huduma zinazozalishwa nchini ili ziweze kutambulika kwa urahisi na kuaminika zaidi katika masoko ya ndani na nje ya nchi.

Akizungumza baada ya kupokea maelezo hayo, Waziri Kapinga alisisitiza umuhimu wa kuendelea kuwajengea uwezo wazalishaji na wafanyabiashara wa ndani ili waweze kuzalisha bidhaa zenye ubora wa juu zinazokidhi mahitaji ya soko la ndani na la kimataifa. Alibainisha kuwa jitihada hizo ni sehemu muhimu ya mkakati wa Serikali wa kuchochea ukuaji wa sekta ya viwanda, kuongeza thamani ya malighafi za ndani na kuimarisha mchango wa biashara katika maendeleo ya uchumi wa Taifa.

Aidha, alieleza kuwa matumizi ya Nembo ya “Made in Tanzania” yana mchango mkubwa katika kujenga utambulisho wa bidhaa za Tanzania, kuongeza imani kwa walaji na kuimarisha ushindani wa bidhaa hizo katika soko la kikanda na kimataifa. Alitoa rai kwa wazalishaji wenye sifa kuendelea kujitokeza kusajili bidhaa zao ili waweze kunufaika na fursa zinazotokana na matumizi ya nembo hiyo.

Maonesho hayo yanatoa fursa kwa wananchi, wawekezaji, wafanyabiashara na wadau mbalimbali kujifunza kuhusu huduma zinazotolewa na taasisi za Wizara ya Viwanda na Biashara pamoja na kujionea mchango wa sera, programu na miradi mbalimbali inayolenga kuharakisha maendeleo ya viwanda, biashara na ujasiriamali nchini.

Uzinduzi wa Sera ya Maendeleo Endelevu ya Viwanda na Sera ya Maendeleo ya Wajasiriamali Wadogo na wa Kati unatarajiwa kuimarisha mazingira ya biashara na uwekezaji, kuongeza tija katika uzalishaji na kuweka msingi imara wa kukuza uchumi shindani unaoongozwa na sekta binafsi.