KONGAMANO LA BIASHARA NA UWEKEZAJI LA ZIWA TANGANYIKA LALETA NEEMA KIGOMA
- April 16, 2026
Kigoma, Tanzania – Aprili 2026
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, amezindua rasmi Kongamano la Biashara na Uwekezaji la Ziwa Tanganyika lililofanyika katika Hoteli ya Lake Tanganyika, mkoani Kigoma.
Akihutubia washiriki, Waziri Mkuu alisisitiza kuwa “pasipo na amani hakuna biashara” na kueleza kuwa Serikali imekuwa ikitekeleza mikakati mbalimbali ya kulinda mazingira ya biashara na uwekezaji, ikiwemo kujenga miundombinu ya kisasa na kuweka mazingira wezeshi ya kiuchumi. Alibainisha kuwa hatua hizi ni msingi wa kuhakikisha Tanzania inabaki kuwa kitovu cha biashara na ushirikiano wa kikanda.
Kongamano hili linalenga kuimarisha nafasi ya Kigoma kama kitovu cha biashara na uwekezaji katika ukanda wa Maziwa Makuu, kuvutia wawekezaji, kuchochea ajira, na kukuza ushirikiano wa kiuchumi baina ya Tanzania na nchi jirani zilizopo kwenye Ushoroba wa Kati. Serikali imeendelea kutekeleza dhamira yake ya kufungua fursa za kiuchumi kupitia uboreshaji wa miundombinu na mazingira rafiki ya biashara kwa manufaa ya wananchi wa Kigoma na Taifa kwa ujumla.
Kongamano la siku mbili, sambamba na maonesho ya siku nne, limeandaliwa na kuratibiwa na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) chini ya uongozi wa Mkurugenzi Mkuu, Dkt. Latifa Mohamed Khamis. Akihutubia washiriki, Dkt. Khamis alieleza dhamira ya TanTrade kuwa daraja la kuunganisha biashara za ndani na nje ya nchi, kuhamasisha uwekezaji na kufungua fursa mpya za kiuchumi.
Aidha, alishukuru wadau wote walioshiriki na aliwaalika kushiriki kikamilifu katika Maonyesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara (DITF 50 Jubilee) jijini Dar es Salaam, akibainisha kuwa ni jukwaa muhimu la kuendeleza ushirikiano wa kibiashara na kuimarisha taswira ya Tanzania kimataifa.