Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania

TanTrade Fostering Business

KIZIMKAZI YAZIDI KUFUNGUA FURSA ZA KIUCHUMI NA MAENDELEO

  • August 13, 2026

Zanzibar | 14 Agosti 2026

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amebainisha kuwa Tamasha la Kizimkazi 2026 limeendelea kuwa jukwaa muhimu la kuchochea shughuli za kiuchumi na kijamii, hususan kwa wananchi wa Kusini Unguja, kupitia fursa zinazojitokeza katika biashara, uwekezaji, utalii na sekta nyingine za maendeleo.

Akizungumza katika kilele cha tamasha hilo, Mhe. Rais alisisitiza kuwa Kizimkazi si tu burudani, bali ni chachu ya maendeleo inayowawezesha wananchi kushiriki moja kwa moja katika shughuli zinazowaongezea kipato na kuboresha maisha yao. Aliongeza kuwa tamasha hilo limekuwa kivutio cha wageni wa ndani na nje ya nchi, hivyo kuchangia kwa kiasi kikubwa katika kukuza sekta ya utalii na kuongeza mapato ya Taifa. 

Aidha, Mhe. Rais aliwapongeza waandaaji, wananchi na wadau mbalimbali kwa mshikamano na ushirikiano wao, akisisitiza kuwa mshirikiano huo ni kielelezo cha umoja na mshikamanano wa Watanzania katika kuendeleza utamaduni na kukuza uchumi wa Taifa.

Katika kuunga mkono jitihada za Serikali za kukuza biashara, uwekezaji na utalii, TanTrade imeshiriki katika kilele cha Tamasha la Kizimkazi 2026 kupitia Naibu Mkurugenzi Mkuu Bw. Freddy Liundi, pamoja na viongozi na watumishi wa Taasisi. Ushiriki huo unaakisi dhamira ya TanTrade ya kushirikiana na wadau katika kuibua na kukuza fursa za biashara, kupanua wigo wa masoko na kuhamasisha bidhaa na huduma za Tanzania.

Zaidi ya hayo, TanTrade imeonesha utayari wa kuendelea kushirikiana na sekta binafsi na wadau wa kimataifa ili kuhakikisha bidhaa za Tanzania zinapata nafasi pana katika masoko ya kikanda na ya kimataifa. Hatua hii inalenga kuimarisha mchango wa sekta ya biashara katika maendeleo ya Taifa na kuunga mkono juhudi za Serikali za kujenga uchumi shindani na endelevu.