Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania

TanTrade Fostering Business

SERIKALI KUENDELEA KUWEKA MAZINGIRA WEZESHI YA MASOKO KWA WAFANYABIASHARA

  • October 22, 2026



21 Oktoba 2026, Babati, Manyara

Serikali kuendelea kutoa ushirikiano na kuweka mazingira wezeshi kwa wafanyabiashara ili kukuza biashara na kuwawezesha kupata masoko ya uhakika ndani na nje ya nchi. Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade), Ephraim Balozi Mafuru, alipokuwa akimwakilisha Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Kapinga, katika kufunga rasmi Maonesho ya Nne ya Biashara ya Tanzanite Manyara Trade Fair, yaliyofanyika katika Viwanja vya Tanzanite Kwaraa, Babati, Mkoa wa Manyara.

Mafuru amesema Serikali kupitia TanTrade itaendelea kushirikiana na wafanyabiashara katika kuwaunganisha na fursa za masoko, pamoja na kuwapatia taarifa na huduma zinazoweza kuwawezesha kukuza biashara zao.Aidha amesisitiza umuhimu wa wafanyabiashara kuzingatia ubora wa bidhaa, ufungashaji bora na matumizi ya chapa ya Made in Tanzania, akieleza kuwa hatua hiyo ni muhimu katika kuongeza ushindani wa bidhaa za Tanzania katika masoko ya ndani na kimataifa, huku ikiimarisha utambulisho wa bidhaa za Tanzania.

Meneja wa Chemba ya Taifa ya Biashara Mkoa wa Manyara, Lerunde Laizer, amesema maonesho hayo yamelenga kuwaunganisha wafanyabiashara na masoko, pamoja na kuwawezesha wajasiriamali kupata maarifa, fursa na taarifa sahihi zinazohitajika katika kukuza biashara zao. 

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chemba hiyo mkoani Manyara, Mussa Msuya, alisema maonesho hayo yamekuwa jukwaa muhimu kwa wajasiriamali kutangaza bidhaa zao, kujenga mahusiano na kukutana na wadau mbalimbali wa biashara. Aidha, aliwahimiza wawekezaji kutumia fursa zilizopo mkoani humo. Takwimu zinaonesha kuwa washiriki wa maonesho wameongezeka kutoka 117 mwaka 2024 hadi 180 mwaka 2026, huku jumla ya watu 14,530, wakiwemo wageni 30 kutoka nje ya nchi, wakitembelea maonesho hayo yaliyokuwa na jumla ya mabanda 74.

Takwimu za uzalishaji zinaonesha uwezo mkubwa wa kiuchumi wa mkoa huo, unaodhihirishwa na uzalishaji wa mahindi tani 440,842 wenye thamani ya shilingi bilioni 198 hadi 265, alizeti tani 113,400 wenye thamani ya shilingi bilioni 136, vitunguu tani 85,000 vyenye thamani ya shilingi bilioni 102 hadi 153, pamoja na Tanzanite inayozalishwa kwa wastani wa kilo 500 hadi 640, yenye thamani ya shilingi bilioni 48.

Maonesho hayo ya Nne ya Tanzanite Manyara Trade Fair yamehitimishwa rasmi leo, yakitoa jukwaa kwa wafanyabiashara, wajasiriamali na wadau mbalimbali kujenga mahusiano ya kibiashara, kutafuta masoko na kuibua fursa mpya za biashara na uwekezaji.