RAIS FEMATA AIPONGEZA TANTRADE KWA KUWAWEZESHA WAFANYABIASHARA KUSHIRIKI MAONESHO MBALIMBALI
- October 4, 2026
02 Oktoba, 2026. Geita.
Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Wadogo wa Madini Tanzania (FEMATA), John Bina, ameipongeza Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) kwa kuendelea kuratibu na kuwawezesha wafanyabiashara na wazalishaji wa bidhaa za Kitanzania kushiriki katika maonesho mbalimbali ndani na nje ya Tanzania.
Bina ametoa pongezi hizo leo, ikiwa ni siku moja kabla ya kufungwa kwa Maonesho ya Tisa ya Teknolojia ya Madini yanayoendelea mkoani Geita, baada ya kutembelea banda la TanTrade na kujionea bidhaa zinazozalishwa na wafanyabiashara na wazalishaji mbalimbali wa Kitanzania. Amesema ushiriki wa TanTrade katika maonesho hayo ni sehemu ya jitihada za kuwaunganisha wafanyabiashara na fursa za masoko pamoja na kuwapatia majukwaa ya kutangaza na kukuza bidhaa zao.
Aidha, Rais huyo wa FEMATA ameeleza kuwa amekuwa akikutana na TanTrade katika maonesho mbalimbali yanayofanyika nchini Tanzania na katika maeneo mengine, akibainisha kuwa uwepo wa Mamlaka hiyo katika maonesho unatoa fursa kwa wafanyabiashara na wazalishaji wa ndani kuonekana na kufikia masoko mapana zaidi. Katika ziara hiyo, Bina alikabidhiwa zawadi ya mvinyo unaozalishwa na wazalishaji wa bidhaa za Kitanzania walioshiriki katika banda la TanTrade.
Maonesho ya Tisa ya Teknolojia ya Madini yanaendelea mkoani Geita huku yakitoa fursa kwa wadau wa sekta ya madini, wafanyabiashara, wazalishaji na wananchi kujifunza, kutangaza bidhaa na huduma, pamoja na kujenga mitandao ya kibiashara. TanTrade inaendelea kushiriki katika maonesho hayo kwa kuwawezesha wafanyabiashara na wazalishaji wa bidhaa za Kitanzania kupata jukwaa la kutangaza bidhaa zao na kuunganishwa na fursa za masoko.